Loading...

Serikali yapiga marufuku malipo ya fedha za kigeni kuanzia tar 1 Januari, 2018

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kwa mara nyingine tena ametoa maagizo kuhusu matumizi ya fedha za kigeni hapa nchini na kusisitiza kuwa utekelezaji wake utaanza rasmi kesho Januari mosi, 2018.

Katika taarifa yake aliyotoa Dar es Salaam jana, Waziri Mpango aliagiza kuwa bei zote hapa nchini zitangazwe kwa shilingi ya Tanzania na kwamba zinajumuisha kodi ya nyumba za kuishi na maofisi, bei ya ardhi, gharama za elimu na afya, bei za vyombo vya usafiri na vifaa vya kielektroniki.

Alisema pia bei ambazo walengwa wake wakuu ni watalii au wateja wasio wakazi, zinaweza kutangazwa kwa fedha za kigeni na malipo yake yanaweza kufanyika kwa fedha za kigeni.

Alizitaja kuwa zinajumuisha gharama za usafirishaji kwenda nchi za nje kupitia Tanzania, gharama za mizigo bandarini kwenda nchi za nje, gharama za viwanja vya ndege na viza kwa wageni na gharama za hoteli kwa watalii kutoka nje ya nchi; na kuwa walipaji wanaotumia fedha za kigeni watambuliwe kwa vitambulisho vyao, kama pasi za kusafiria na nyaraka za usajili kwa makampuni.

Dk Mpango aliagiza pia viwango vya kubadilishana fedha vitakavyotumika katika kuweka hizo bei katika sarafu mbili, viwekwe wazi na visizidi vile vya soko; na kuwa ifahamike wazi kuwa ni mabenki na maduka ya fedha za kigeni tu yanayoruhusiwa kupanga viwango vya kubadilisha fedha kutokana na ushindani katika soko la fedha za kigeni.

Hata hivyo, Waziri Mpango alisema mkazi yeyote wa Tanzania, asilazimishwe kulipia bidhaa au huduma yoyote hapa nchini kwa fedha za kigeni. Waziri huyo aliviagiza vyombo vya dola, viwachukulie hatua za kisheria wale wote watakaobainika kukiuka maagizo haya ya serikali
Serikali yapiga marufuku malipo ya fedha za kigeni kuanzia tar 1 Januari, 2018 Serikali yapiga marufuku malipo ya fedha za kigeni kuanzia tar 1 Januari, 2018 Reviewed by Zero Degree on 12/31/2017 03:26:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.