Loading...

Bandari ya Dar es Salaam yapanuliwa


MAMLAKA ya Bandari Tanzania (TPA) imesema kukamilika mradi wa upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam utawezesha mamlaka hiyo kuwa na uwezo wa kupokea meli yenye urefu wa mita 306 badala ya mita 245 zinazoingia sasa.

Mradi huo wa Dar es Salaam Maritime Gateway Project (DMGP) umeanza kutekelezwa kwa kuboresha gati namba moja mpaka saba kwa thamani ya Sh bilioni 336 na unatarajiwa kukamilika Februari 2020.

Hayo yalibainishwa jana jijini humo na Mkurugenzi wa TPA, anayeshukughulikia Miundombinu, Karim Mattaka wakati akizungumza kuhusu uboreshwaji wa bandari hiyo.

Alisema mradi huo utafanya marekebisho katika gati namba moja mpaka namba saba ikiwa ni pamoja na kuongeza kina pamoja na miundombinu ya bandari ikiwa ni pamoja na kuboresha ulinzi.

Alisema uingiaji wa meli zenye urefu mkubwa katika bandari hiyo ni mgumu kwa kuwa haina uwezo wa kupokea meli hizo kutokana na mita za urefu katika eneo hilo.

“Manahodha wetu wanapofika ni lazima wavizie maji yakiwa juu sana ndio waingie lakini wakikosea wanaweza kuingiza meli kwenye mchanga, meli kubwa ambayo imewahi kuingia ina urefu wa mita 261 na hii imetokana na umahiri wa manahodha wetu hivyo kukamilika kwa upanuzi huu kutawezesha meli zenye urefu wa mita 305 kutia nanga badala ya mita 245,” alisema Mattaka.

Alisema mbali na Bandari ya Dare es Salaam, mamlaka hiyo inaboresha bandari ya Mtwara na Tanga ili kuziongezea uwezo wa kupokea na kupakuwa mzigo kwa meli kubwa.

Aliongeza kuwa kwa bandari ya Mtwara tayari kuna mradi mkubwa wa ujenzi wa gati ya kisasa yenye urefu wa mita 300 na kuongeza kina katika maeneo machache wenye gharama ya Sh bilioni 136 ambao unatarajiwa kukamilika mwanzoni mwa mwaka 2019.

Mattaka alisema uboreshwaji wa bandari hiyo itasaidia kuongezea uwezo bandari kuwa na uwezo wa kupokea kontena 400,000 kwa mwaka na itakuwa ya kisasa na kuwezesha bandari hiyo kushindana na bandari zilizopo jirani.

Alisema kwa bandari ya Tanga, wana mpango wa kufanya utafiti wa eneo la ujenzi wa kwa ajili ya meli kubwa za mafuta na pampu za kuhifadhi mafuta ili kuwezesha meli hizo kushusha mafuta.

Aliongeza kuwa mbali na ujenzi kwa ajili ya mafuta pia wamejipanga kuboresha bandari hiyo ili kuwezesha nchi za Afrika Mashariki kutumia bandari hiyo kusafirisha mizigo yao.

Mattaka alisema mbali na kuboresha bandari hizo kubwa pia wana mpango wa kuboresha bandari zote zilizopo katika ukanda wa maziwa ili kuziongezea tija na uwezo.

Source: Habari Leo
Bandari ya Dar es Salaam yapanuliwa Bandari ya Dar es Salaam yapanuliwa Reviewed by Zero Degree on 2/23/2018 08:03:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.