Loading...

TTCL kutumia bilioni 44 kufukisha intaneti majumbani


Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) linatarajia kutumia Sh44.7 bilioni kusambaza intaneti ya kasi kubwa hadi majumbani kupitia huduma mpya iitwayo Fiber Connect Bundle.

Hayo yamebainishwa leo, Jumanne Februari 27, 2018 na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Waziri Kindamba aliyebainisha kuwa kupitia huduma hiyo mteja atapata intaneti ya kasi isiyo na ukomo kwa gharama ya kuanzia Sh100,000 hadi Sh200,000 kwa mwezi.


“Pia, atapata simu ya mezani bure yenye huduma ya wifi pamoja na muda wa maongezi bure na kadi ya simu,” amesema Kindamba.

“Kwa kuanzia mradi huu, tunatarajia kufikisha huduma katika nyumba 500 zilizopo Mikocheni na nyingine 500 za Mbezi Beach jijini hapa. Zaidi ya nyumba 200 zilizopo eneo la Medeli mkoani Dodoma nazo zimo kwenye mpango, baadaye huduma hii itaendelea kusambazwa nchi nzima.” 

Amebainisha kuwa uwekezaji katika sekta ya mawasiliano ni wa gharama kubwa, lakini shirikia hilo litaendelea kufanya kila liwezalo kuwafikia Watanzania wote kwa kuboresha mtandao wa simu na intaneti kwa gharama nafuu.

Mkuu wa Ufundi wa shirika hilo, Cecil Francis amesema muda wa majaribio ya mradi huo ni miezi mitatu kisha huduma hiyo itaanza kutolewa katika majiji yote ya Tanzania Bara pamoja na Unguja katika awamu ya kwanza.
  

“Awamu ya kwanza inatarajia kugharimu kati ya Dola 15 milioni za Marekani (zaidi ya Sh33 bilioni) hadi Dola 20 milioni (zaidi ya Sh44 bilioni). Utekelezaji wake tayari umeanza tangu Februari Mosi na baada ya siku 90 tutaendelea na maeneo mengine tulivyoyapa kipaumbele,” amesema Francis.
TTCL kutumia bilioni 44 kufukisha intaneti majumbani TTCL kutumia bilioni 44 kufukisha intaneti majumbani Reviewed by Zero Degree on 2/27/2018 11:15:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.