Loading...

Vyeti vya kuzaliwa sasa kutolewa papo hapo

Kaimu Mtendaji Mkuu wa Rita, Emmy Hudson
WAKALA wa Usajili, Ufisili na Udhamini (Rita) umeanza kutoa vyeti vya kuzaliwa na vifo mara baada ya tukio kwenye vituo 60 vya mikoa ya Dar es Salaam, Shinyanga na Geita.

Hayo yalibainishwa jana na Kaimu Mtendaji Mkuu wa Rita, Emmy Hudson, wakati wa ziara ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Prof. Sifuni Mchome makao makuu ya wakala huo. 

Prof. Mchome alifanya ziara hiyo kujionea mfumo wa usajili wa vizazi na vifo kupitia mradi wa maboresho ya miundombinu ya Tehama, unaofadhiliwa na Benki ya Dunia (WB).

Hudson alisema kwa sasa mtoto anapozaliwa na kabla mama hajatoka hospitali, hupata cheti na kwa kifo Rita hukitoa kabla ya mwili kuondolewa kwenye hospitali zenye mfumo.

"Lengo kuu la maboresho ni kuwezasha matukio ya vizazi na vifo kufanyika kwa ufanisi zaidi na karibu zaidi na wananchi, na kuimarisha miundombinu ya usajili, usafirishaji taarifa, uhifadhi wa taarifa pamoja na matumizi ya taarifa ndani na nje ya wakala," alisema Hudson. 

Kwa mujibu wa mtendaji huyo, mfumo huo umeanza kwenye vituo 60 vya majaribio, madawati manne ya usajili wa Rita makao makuu, kuboresha mfumo wa kielektroniki, kuboresha mfumo wa zamani wa utafutaji taarifa na kuweka mfumo maalum wa kutoa namba za kuzaliwa.
  

"Hatua iliyofikiwa hadi sasa ni mfumo maalum wa namba za usajili wa vizazi kutumika, kuharakisha utafutaji wa taarifa za zamani, majaribio ya usajili wa ndoa na talaka, na umeunganishwa na mfumo wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida)," alisema. 

"Pia tumeunganisha na mfumo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) ili kubadilishana taarifa." 

Mkurugenzi wa Tehama wa Rita, Cathbert Simalenga, alisema mradi huo ulioanza Novemba mwaka jana, umegharimu zaidi ya Dola za Marekani milioni tano (sawa na Sh. bilioni 12), ambazo zimeweka mfumo wa kanzi data makao makuu, kwenye vituo na kituo cha wakala wa serikali mtandao.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, vituo 40 vinaweza kusajili na kutoa vyeti siku hiyo hiyo na 20 vinasajili pekee, na kwamba Rita ina ofisi 139 nchini ambazo kati yake 66 zimefungwa mfumo wa Tehama zikiwa na vifaa vya kisasa.

Prof. Mchome aliitaka Rita kuharakisha usajili wa vizazi ili kuwezesha Watanzania wengi kuwa na vyeti vya kuzaliwa au kusajili matukio muhimu ya maisha yao kwa kutumia teknolojia rahisi.

"Tanzania ni kubwa (na) watu wanazaliwa, kufa na kuoana kila siku," alisema na kusikitika "wanapata changamoto ya kufuatilia vyeti". 

"Matukio muhimu ya binadamu ni lazima yaingie katika kumbukumbu ili kuiwezesha serikali kupanga vyema mipango yake."
Vyeti vya kuzaliwa sasa kutolewa papo hapo Vyeti vya kuzaliwa sasa kutolewa papo hapo Reviewed by Zero Degree on 2/09/2018 07:02:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.