Loading...

Wanaokwepa kunyonyesha watoto kuundiwa sheria kali

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk Rehema Nchimbi
MKUU wa Mkoa wa Singida, Dk Rehema Nchimbi ametoa miezi minne kuanzia sasa kwa uongozi wa vijiji na kata kuhakikisha wanatunga sheria ndogo ya kunyonyesha ili kuondokana na tatizo la ukosefu wa lishe kwa watoto mkoani hapo.

Dk Nchimbi alitoa agizo hilo juzi wakati wa hafla ya kukabidhiwa vifaa vya kutambua hali ya lishe kwa watoto na akinamama wajawazito katika kijiji cha Saranda wilayani Manyoni.

Alilazimika kutoa agizo hilo baada ya kusomewa taarifa inayoonesha kuwa ni asilimia 54 tu ya watoto mkoani Singida ndio hubahatika kunyonyeshwa maziwa ya mama pekee kwa kipindi cha miezi sita.

Alisema kuwa suala la kunyonyesha siyo la hiari kwa kuwa kutokufanya hivyo kunahatarisha afya ya mtoto. “Kunyonyesha ni lazima. Wenyeviti wa vijiji na kata hakikisheni mmetunga sheria ndogo kwa ajili ya kudhibiti akinamama wote wasionyonyesha watoto wao kulingana na taratibu za afya.”

Nchimbi alisema kuwa ulazima huo usibakie kuwa ni wa majukwaani tu bali utekelezwe kisheria na atakayepatikana aadhibiwe, hata hivyo, mhakikishe adhabu hiyo haisababishi mama kumkimbia mtoto.

Aidha, Dk Nchimbi aliagiza pia itungwe Sheria ndogo kwa ajili ya kuwapatia wanafunzi chakula cha mchana wawapo shuleni. Aliwataka pia viongozi wa dini kuhubiri suala la lishe akidai kuwa mahubiri hayawezi kumwingia vyema muumini asiye na lishe njema.
Wanaokwepa kunyonyesha watoto kuundiwa sheria kali Wanaokwepa kunyonyesha watoto kuundiwa sheria kali Reviewed by Zero Degree on 2/04/2018 07:37:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.