Loading...

Mzee wa miaka 68 akamatwa na nyaraka za Serikali


Mtu mmoja mkazi wa Yombo Kilakala anayefahamika kwa jina la Selemani Masudi (68) anashikiliwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa tuhuma za kukutwa na nyaraka mbalimbali za serikali, ikiwemo mihuri 53 na vitambulisho vya uraia 26.

Hayo yamesemwa leo Machi 16, 2018 na Kamishna wa Polisi Kanda Maaalumu ya Dar es Salaam, SACP Lazaro Mambosasa wakati akizungumza na wanahabari.

Akifafanua kuhusu tukio hilo, amesema mtuhumiwa huyo alikamatwa akiwa nyumbani kwake maeneo ya Yombo Kilakala katika harakati za uandaaji wa nyaraka hizo kwa ajili ya wateja wake, baada ya makachero wa polisi kupata taarifa zake kutoka kwa raia wema.
  

“Tarehe 13 Machi jeshi la polisi lilipata taarifa kupitia kituo cha intelejensia kwamba kuna kundi linalojihusisha na kutengeneza vyeti feki, mihuri bandia na nyaraka za serikali na kisha nyaraka hizo kutumia isivyo halali, baada ya taarifa hizo makachero walianza ufuatiliaji mara moja, wakaenda kwenye nyumba ya mtuhumiwa,” amesema na kuongeza. 

“Alikutwa na nyaraka mbalimbali na jumla ya mihuri 53, ilikuwa pamoja na nyaraka za Baraza la Mitihani NECTA, mihuri ya VETA, Vyuo vikuu vya Dar es Salaam, SUA, OUT, NIT, IFM, Mtwara na mhuri wa TRA, Bodi ya Uhasibu NBAA, RITA, JKT Makao Makuu, Mahakama ya Kisutu, Wizara ya Mali Asili na Utalii, pia kibali cha mazishi na kadi 26 za uraia Tanzania.”

Amesema mtuhumiwa huyo anaendelea kuhojiwa, na kwamba mahojiano yakikamilika atapelekwa mahakamani kujibu shitaka la kukutwa na nyaraka mbalimbali za serikali kinyume na sheria.
Mzee wa miaka 68 akamatwa na nyaraka za Serikali Mzee wa miaka 68 akamatwa na nyaraka za Serikali Reviewed by Zero Degree on 3/16/2018 06:14:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.