Loading...

Jaji Mkuu aionya TLS


JAJI Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma amekitaka Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), kutojiingiza kwenye siasa wala masuala ya harakati.

Amesema endapo chama hicho kitajiingiza katika masuala hayo hawatapata ushirikiano.

Profesa Juma amewaeleza waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa, chombo hicho kipo huru kufanya kazi yake kitaaluma kwa maslahi ya wananchi.

"TLS ni chama cha umma na sio binafsi kama watu wanavyosema hivyo hakipaswi kujiingiza katika masuala ya harakati kwani hatutawapa nafasi ya kutushauri," amesema.

Amesema, TLS ikitaka kushirikiana na mahakama wanapaswa kubaki katika kazi zao, wasipotaka watafanya majukumu yao lakini bila ushirikiano.

Jaji Mkuu amesema baadhi ya majukumu ya TLS ni kuboresha taaluma ya sheria na hiyo si kazi binafsi, ni kazi ya umma ili kuendeleza wanachama waendane na mabadiliko ya sheria.

Alifafanua kuwa yeye anamamlaka ya kutunga sheria ndogo ndogo lakini akitunga lazima ziende kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili azipitie, endapo kipo chombo chochote kinachotengeneza kanuni bila kupitia kwa mwanasheria wanajidanganya.

"TLS ina majukumu ya kitaifa ambapo inatakiwa kuisaidia Serikali, Bunge na Mahakama katika masuala mbalimbali ya sheria, hivyo hamtaweza kuisaidia serikali kwa kulumbana, hiki si chama binafsi inatakiwa kurudi katika malengo ya kuanzishwa kwake kwa mujibu wa sheria," amesema.
Jaji Mkuu aionya TLS Jaji Mkuu aionya TLS Reviewed by Zero Degree on 4/25/2018 11:35:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.