Loading...

Bashe alivyotikisa Bunge kukiukwa Ilani ya CCM


Tangu kuanza kwa Bunge la Bajeti Aprili 3, moja kati ya hoja zilizotikisa chombo hicho cha kutunga sheria ni ujenzi wa reli ya kisasa (SGR).

Mjadala wa bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano uliohusisha zaidi ya wabunge 20, uilimuweka katika hali ngumu Waziri Makame Mbarawa hasa kutokana na hoja ya mbunge wa Nzega (CCM), Hussein Bashe aliyesema ujenzi wa reli hiyo ulioainishwa katika bajeti, ni kinyume na Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

Katika bajeti hiyo, Serikali imetenga Sh1.5trilioni ambazo ni fedha za ndani kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa reli ya kati ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro (km300) na Morogoro hadi Makutopora (km422), na Sh1.4 trilioni zitatumika.

Pia, Wizara imetenga Sh100 bilioni kwa ajili ya kuanza ujenzi wa reli ya Isaka-Rusumo (km371) kwa kushirikiana na Serikali ya Rwanda.

Bashe aliibua hoja hiyo wakati Bunge lilipokaa kama kamati kupitisha bajeti hiyo na kuungwa mkono na wabunge wa upinzani na CCM.

Waliomuunga mkono ni Hawa Ghasia (Mtwara Vijijini-CCM), James Mbatia (Vunjo-NCCR-Mageuzi), John Heche (Tarime Vijijini-Chadema), Magdalena Sakaya (Kaliua-CUF) na Daniel Nsanzugwako (Kasulu Mjini-CCM).

Katika hoja yake, Bashe alisema kwa mujibu wa Ilani ya CCM, ujenzi wa reli hiyo ni kutoka Dar es Salaam-Tabora, Tabora-Mwanza, Tabora-Kigoma, Kaliua-Mpanda-Kalemii na Uvinza-Msogati na kushangazwa na uamuzi wa kutengwa Sh100bilioni za ujenzi wa reli kutoka Isaka kwenda Rusumo, ambako ni mpaka wa Tanzania na Rwanda.

Bashe alitaka Sh100 bilioni zihamishwe na kupelekwa katika ujenzi wa reli hiyo kutoka Makutopora hadi Tabora, akisisitiza kuwa reli ni lazima ijengwe kwanza nchini, kama inaunganishwa na nchi nyingine, ni vyema zikawa nchi zinazopitisha zaidi mizigo yake Tanzania. Alisema Rwanda haipitishi mizigo mingi kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Kutokana na mvutano ulioibuka bungeni huku wabunge wakiitaja nchi ya Rwanda, Naibu Spika, Dk Tulia Ackson alilazimika kuwakatisha na kuwataka kutoitaja nchi hiyo wala jina la mtu, ili kulinda uhusiano wa kidiplomasia.

Ilivyoanza

“Kama waziri hataniridhisha nitashika shilingi. Hoja iliyopo mbele yetu ni kwamba ilani ya CCM imesema wazi tunajenga reli ya kisasa; Dar es Salaam- Tabora, Tabora-Mwanza, Tabora-Kigoma, Kaliua-Mpanda-Kalemii, Uvinza-Msongati,” alisema Bashe. 

“Wanachokifanya Serikali sasa ni mawazo yaliyobuniwa na ADB (Benki ya Maendeleo Afrika) chini ya mtu anaitwa Kaberuka ambaye alitengeneza mpango wa Northern Route (njia ya Kaskazini) kutoka Mombasa-Kigali, Dar es Salaam-Isaka hadi igali, ili kuifanya Kigali kuwa kitovu cha kusafirisha mizigo.” 

Alisema mpango huo utaifanya Rwanda kuwa kitovu cha kusafirisha mizigo kwa maelezo kuwa ili mizigo ya Bukavu (DRC) na Burundi kusafirishwa kupitia Rwanda, ni lazima ijengewe bandari kavu nchini humo.

“Nashindwa kuelewa kwanini wataalamu hawalioni (hili) wakati inaeleweka kabisa mtaji wetu si Bukavu, mtaji wetu ni mashariki na magharibi ya Congo na Burundi,” amesema. 

“Waziri anasema haujafanyika upembuzi yakinifu kutoka Tabora kwenda Kigoma. Sasa upembuzi kanikifu kutoka Isaka kwenda Rwanda umefanyika lini? Ni ile (upembuzi) ya ADB iliyofanywa na Kaberuka. Hii si sawa kwa Taifa letu, hii ni sawa kwa chama chetu.” 

Alisema iweje nchi isiwe na fedha ya kujenga reli kutoka Makutopora kwenda Tabora ila iwe na fedha za ujenzi kutoka Isaka kwenda Rwanda.

“Sasa tukisafirisha kwa reli hii kwenda mpaka Makutopora halafu kuanzia hapo tutabeba kwa helkopta, inakuwaje hii? Lazima tufahamu tutashindana na bandari ya Mombasa. Waziri, Sh100bilioni iondoeni na uirejeshe Makutopora na Morogoro maana hayo maeneo ndio tunayotaka kuweka fedha tukamilishe hatua ya pili na ya tatu mwaka 2020,” amesema. 

Baada ya hoja hiyo, Dk Tulia alizuia wabunge na Profesa Mbarawa kutaja jina la Rwanda na kumpa nafasi waziri huyo kutoa ufafanuzi wa maelezo ya Bashe

Katika ufafanuzi wake Profesa Mbarawa alisema: “Tunamalizia upembuzi yakinifu kutoka Tabora-Kigoma kwa ajili ya ujenzi. Sasa hatuwezi kusema tunajenga kwa kiasi gani. Lazima jambo hilo likamilike ndio tutajua kiasi tutakachotumia kujenga. 

“Kuchukua kontena moja kutoka Dar es Salaam hadi Kigali tunatumia dola 4,200 za Kimarekani, kontena hiyohiyo kutoka Mombasa hadi Rwanda tunatumia dola 4,700. Bado ni gharama kutumia njia ya kule kuliko huku. Mfanyabiashara anayetaka faida hawezi kutumia njia ile (ya Mombasa-Rwanda),” alisema Mbarawa. 

Lakini Bashe alipinga maelezo hayo na kushika shilingi ya waziri, hivyo kutoa mwanya kwa wabunge kujadili suala hilo.

Mjadala ulivyokuwa

Akizungumzia suala hilo Mbatia, alisema: “Naunga mkono hoja ya Bashe. Ukitaka kufanya mradi wowote ule tangu unapoanza wazo, lazima uwe na mpango mkakati wa mradi wote.” 

“Hapa tunazungumzia Bandari ya Dar es Salaam na ujenzi wa reli. Mradi huu (wa reli) tunawekeza fedha nyingi sana na Bunge ndio linasimamia Serikali na kuishauri. Ingekuwa vyema ili kuondoa utata unaojitokeza. Serikali kwa kutumia hoja ya Bashe ifanye utaratibu wa maslahi ya humu ndani kwanza (nchini).” 

Mbatia alisema msingi mkuu wa ujenzi wa reli hiyo ni mizigo na kwamba badala ya kujenga bandari kavu Rwanda, Serikali iimarishwe Bandari ya Dar es Salaam na reli hiyo.

“Tuangalie maslahi mapana ya Tanzania kwanza kabla ya wengine. Tuhakikishe mradi mzima unawekwa wazi na kujulikana,” alisema Mbatia. 

Kwa upande wake, Heche, mbali na kuunga mkono hoja ya Bashe, alisema hata kwa hesabu za darasa la pili mzigo unaokwenda Rwanda na Burundi ni asilimia 12 wakati unaokwenda Congo ni asilimia 36.

“Hao Rwanda wamefanikiwa, wameleta watu wajanja wanataka kuhamisha uchumi wa nchi yetu kujenga nchi yao. Suala hili linagharimu fedha nyingi sana kama ulimsikiliza Rais (John Magufuli) alisema wameshatoa Sh7trilioni kwa ajili ya ujenzi wa reli hii,” alisema. 

“Ila kwenye kitabu cha bajeti, fedha zilizoombwa ni Sh1.5trilioni. Kipi sahihi, alichosema Rais au kilichoandikwa kwenye kitabu cha bajeti. Inashangaza na kuchanganya kwanini tunakimbilia huko Rwanda?” 

Naye Nsanzugwako, ambaye ni mjumbe wa kamati ya Bunge ya Miundombinu, alibainisha kuwa katika kamati yake mjadala kuhusu ujenzi huo pia ulikuwa tofauti.

“Tulijadili jambo hili na hoja ilikuwa reli hii ijengwe kwanza kipande cha Tabora-Kigoma, lakini waziri na timu yake wakasema hapana kwamba mzigo mkubwa upo Uganda. Wakasema reli itoke Tabora kwenda Mwanza tukasema kwa takwimu hizi ni kitu chema,” alisema. 

“Ila mzigo mwingine mkubwa upo DRC na ukichanganya mzigo wa Burundi unakuwa mkubwa kuliko mzigo ulioko Uganda. Kwa hoja hiyo tukaogopa tusianze kugombana, tukakubaliana ujenzi wa Tabora-Mwanza.” 

Alisema walikubaliana awamu nyingine iwe ujenzi wa Tabora-Kigoma.

“Leo kinachonishangaza, hizi Sh100 bilioni ni bora tuziweke Makutopora kwenda Tabora, kuliko Isaka kwenda Rwanda. Sisi tunazaliwa maeneo ya Kigoma, mtaji wa reli hii ni mzigo unaotoka DRC kuja Bandari ya Kigoma ili reli iwe na faida. Hizi Sh100 bilioni kwanini ziende Rwanda? 

“Naunga mkono hoja ya Bashe. Ujenzi wa reli hii nia yake ni kuondoa msongamano Bandari ya Dar es Salaam jambo ambalo waziri anajua. Upembuzi yakinifu ambao ulipaswa kufanywa ni mzigo unaotoka bandari hiyo mwingi unaelekea nchi gani ili reli tupeleke kwa jirani anayetupa mzigo mkubwa,” amesema Ghasia. 

Kwa upande wake Sakaya amesema ujenzi wa reli ya kati unapaswa kulenga kusafirisha mizigo na mazao, “Sh100bilioni zinaweza kuanza mchakato wa ujenzi wa reli kutoka Dodoma kwenda Tabora. Fedha hizi zipelekwe katika nchi ambazo zitasafirisha mizigo zaidi kupitia reli yetu, fedha hii ihame.”

Mbunge wa Karagwe (CCM), Innocent Mashungwa alipingana na hoja ya Bashe na kubainisha kuwa alishiriki katika upembuzi yakinifu wa madini ya Nickel mkoani Kagera na kubainisha kuwa ujenzi wa reli hiyo utasaidia kusaidia uchimbaji wa madini hayo.

Naye mbunge wa Kibakwe (CCM), George Simbachawene aliungana na Bashungwa kupinga hoja hiyo ya Bashe.

“Naielewa hoja ya Bashe mipango ya kuijenga reli ya Kigoma-Tabora ipo lakini hakuna uwezekano wa kuepuka kujenga reli ya Isaka-Kigali.” 

“Upembuzi yakinifu ukikamilika na hii inajengwa kuna haja gani ya kuondoa hii fedha. Naomba sana uamuzi wa Serikali wenye maudhui makubwa uachwe kwa sababu Serikali imeshasema upembuzi yakinifu ukikamilika reli itajengwa kwenda Kigoma.” 

Mbarawa atoa ufafanuzi

Baada ya wabunge kujadili, Profesa Mbarawa alirejeshewa kijiti kutoa ufafanuzi zaidi na kubainisha tofauti na viwango vya mizigo vya nchi mbalimbali inayopita Tanzania.

“Tunaanzia mzigo kwa Rwanda kuna tani milioni 1.1. mzigo wa Congo unaokuja Tanzania unatoka Kaskazini na Kusini mwa nchi hiyo. Kaskazini ya Congo maeneo ya Bukavu na Goma kuna tani 750,000. Upande mwingine Kusini yaani Lubumbashi kuna tani 3milioni ambazo zinagawiwa katika nchi kama tano; Afrika Kusini, Namibia, Angola, Msumbiji na mzigo unaokuja Tanzania kupitia Zambia ni tani 780,000 tu,” alisema. 

“Ukija upande wa Tanzania tuna Nickel tani 36.4milioni. Reli tunajenga Isaka mpaka Rusumo, hatujengi kutoka Rusumo kwenda Kigali, Rwanda. Huwezi kujenga reli kwa Sh100bilioni. Hizo fedha tumeweka kwa ajili ya kulipa fidia na upembuzi yakinifu.” 

Bashe akomalia hoja yake

Baada ya maelezo hayo, hoja ilirejeshwa kwa Bashe kwa ajili ya kuhitimisha.

“Naomba nieleweke. Hoja yangu ni kwa nia njema na maslahi ya nchi yetu. Waziri katoa takwimu kasema kusafirisha kontena moja ni dola 4,200 kutoka Dar kwenda Rwanda na kutoka Mombasa kwenda Rwanda ni dola 4,700 lakini hajamalizia kwamba hizi ni gharama za kusafirisha kwa maroli sio treni,” alisema. 

Kuhusu madini ya Nickel, alisema: “Najua tuna hazina ya Nickel Kabanga ila lazima twende na taarifa za dunia. Migodi mingi ya Nickel duniani imefungwa kwa sababu bei na thamani na madini haya imeshuka.” 

“Ikifika mahali kama hatutoelewana nataka niingie katika kumbukumbu za Bunge kwamba hili jambo nimelisema ila kama tutaamua kwenda nalo kwanini tusiweke sehemu ambayo tunakwenda kupata mapato.” 

Hata hivyo, Bashe alipomaliza maelezo yake, Dk Tulia alimtaka kueleza msimamo wake kama harejeshi shilingi ya waziri ili Bunge liende katika hatua ningine, mbunge huyo alirejesha shilingi na hoja hiyo kuishia hapo.

Source: Mwananchi
Bashe alivyotikisa Bunge kukiukwa Ilani ya CCM Bashe alivyotikisa Bunge kukiukwa Ilani ya CCM Reviewed by Zero Degree on 5/02/2018 03:14:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.