Loading...

Msekwa, Kafulila, Baregu waguswa uteuzi wa Bashiru


WASOMI na wanasiasa wameunga mkono uteuzi wa Dk Bashiru Ally kuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kumuelezea kuwa ni mtu anayeifahamu vyema siasa, anayependa ujamaa na asiyeyumbishwa katika mambo ya msingi.

Dk Bashiru ambaye anakabidhiwa rasmi leo ofisi hiyo ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahaman Kinana, aliyeomba kung’atuka mpaka juzi alipoteuliwa kushika wadhifa huo mpya, alikuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kama mtaalamu wa mambo ya siasa, lakini pia ndiye Mwenyekiti wa Tume ya Kuhakiki mali za CCM iliyoundwa na Rais John Magufuli Desemba 20, 2017.

Kwa mujibu wa taarifa ya Habari Leo, aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Pius Msekwa alisema wao kama Wazee wa Chama, wameunga mkono uteuzi huo, kwa kuwa ni wakati muafaka wa kuwa na Katibu Mkuu mwenye uwezo wa kusimamia vizuri rasilimali za Chama.

Msekwa alisema kwamba ana imani na Dk Bashiru kuwa atadhibiti uhalifu wa mali za Chama usitokee tena ili chama hicho kiweze kuwa katika hali nzuri ya kifedha.

“Ingawa CCM tuko vizuri kisiasa, lakini kifedha tulikuwa na hali mbaya kutokana na wizi na ubadhirifu wa mali. Matarajio yangu ni kwamba Dk Bashiru atakuwa na uwezo wa kuifanya CCM kuwa na hali nzuri ya kiuchumi kwa kudhibiti uhalifu usitokee tena,” alieleza Msekwa.

Hoja hiyo ya Msekwa iliungwa mkono na aliyewahi kuwa Mbunge wa Kigoma Kusini kwa tiketi ya NCCR Mageuzi, David Kafulila aliyesema kuwa anapoitazama safu ya uongozi wa CCM ilivyo sasa, anauona mwisho wa CCM mazoea, CCM upigaji dili na CCM kichaka cha wezi.

Kafulila alisema kuwa safu ya uongozi wa CCM Taifa chini ya Mwenyekiti Rais Magufuli, Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Philip Mangula, Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein na kupatikana kwa Dk Bashiru katika nafasi ya ukatibu mkuu, anaona kuwa ni mapinduzi makubwa na kuzaliwa kwa CCM Mpya.

“Mwaka 2008 aliyekuwa Balozi wa Norway Tanzania, alipata kusema kwamba changamoto kubwa inayoikabili vyama vya upinzani Tanzania ni uwezo wa CCM kujibadilisha katika kukidhi mahitaji ya wakati. Kupatikana kwa Rais Magufuli mwaka 2015 inanikumbusha kauli hiyo,” alisema Kafulila na kuongeza

“Lakini kupatikana kwa Dk Bashiru na ninapoona CCM pale juu amekaa Dk Magufuli, Dk Shein na Mangula ndipo dhana ya CCM Mpya na kujivua gamba inapoonekana; wasioamini katika CCM Mpya sasa watabaki na mning’inio (hangover).”

Kwa mujibu wa Kafulila, Dk Bashiru ni mtu mwenye misimamo ya kijamaa na misimamo ya Mwalimu Julius Nyerere, na ndiyo maana ameweza hata kufanikisha kazi ngumu ya kufuatilia mali za CCM katika mazingira ambayo pengine hayakuwa salama sana kwake.

Alisema hakuna mwanasiasa asiyemfahamu Dk Bashiru, kwa kutoa ushauri wa kisiasa kwa vyama mbalimbali kuhusu namna ya kuendesha siasa nchini, lakini pia ni mtu safi, mwadilifu, mkweli, mwenye nguvu thabiti, asiyeyumba anaposimamia maslahi ya nchi na anachukia ufisadi.

“Safu hii ya uongozi ni uthibitisho kweli CCM ni Chama cha Mapinduzi. Kazi aliyoifanya Dk Bashiru ya kuhakiki mali za Chama akiwa hana mamlaka wala kinga yoyote, ilikuwa ngumu sana kwa yeyote anayefahamu namna upigaji dili ulivyokuwa umejisuka ndani kwa miongo mingi.

“Hivyo hali ya sasa kwa yeye kupewa ukatibu mkuu akiwa na jukumu la kwanza kufanyia kazi ripoti yake, tutegemee mafanikio makubwa ya maazimio ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC),” alieleza Kafulila.

Kuhusu tabia yake ya kutoa ushauri wa kisiasa kwa vyama mbalimbali vya siasa nchini, aliyewahi kuwa mgombea urais kupitia chama cha UPDP, Fahamy Dovutwa alimtaka Dk Bashiru kuendelea kushirikiana na vyama hivyo, pale watakapomuhitaji.

Dovutwa alisema kuwa Dk Bashiru ni mzoefu wa siasa lakini pia ni mwanasiasa. Alisema kuwa CCM wamempata mtu sahihi, kwa kuwa anaifahamu historia ya nchi na anakielewa CCM vizuri.

Alisema kazi aliyopewa ya kufuatilia mali za CCM, imempa picha nzuri ya namna Chama kilivyo, lakini alimtaka awe anaitikia wito wa vyama vingine pale watakapomuhitaji, kwa kuwa vyama hivyo vinataka taaluma yake tu na siyo kitu kingine.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Profesa Mwesiga Baregu alimtaka Dk Bashiru kuleta mawazo ya kukuza demokrasia nchini, kwa kuwa ana fikra nzuri na pevu katika masuala mengi, lakini pia anaamini katika uhuru wa maoni na mawazo.

Kwa upande wake, alipoulizwa ni kwa namna gani, ameupokea uteuzi huo wa kuwa Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru alisema kuwa atazungumzia jambo hilo leo, siku ambayo anakabidhiwa rasmi Ofisi ya Katibu Mkuu wa Chama.

Aliongeza kuwa ni haki ya wananchi kujua maoni yake. Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana alisema kuwa hana shaka na uwezo wa Dk Bashiru katika kuyamudu na kuyatekeleza majukumu yake hayo mapya ya ukatibu mkuu wa chama.

Dk Bana alisema kuwa anamfahamu Dk Bashiru vizuri, kwa kuwa alikuwa mwanafunzi wake, lakini pia wamefanya kazi pamoja UDSM, hivyo ana uwezo wa kuongoza. Pia, alisema taaluma yake ya Sayansi ya Siasa na Utawala, itamsaidia katika kuchambua na kuchanganua mambo kwa kina na kutoa ushauri kwa uongozi wa juu wa Chama.

“Dk Bashiru nimemfundisha, namfahamu kuwa ni mzalendo wa kweli, ana uchungu na nchi, ana mtazamo wa kuwafikiria wanyonge, lakini pia ni muumini wa Majumui ya Afrika,” alisema Dk Bana.

Kwa mujibu wa Dk Bana, changamoto ambayo Dk Bashiru atakutana nayo muda mfupi ujao ni uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwakani na uchaguzi mkuu mwaka 2020.

Alisema anachotakiwa kufanya ni kuongoza vyema Sekretarieti ya CCM kuanzia juu hadi ngazi ya Shina ili Chama kiendelee kufanya vizuri.

Aliongeza kuwa Dk Bashiru hana budi kufuata nyayo za mtangulizi wake, Abdulrahman Kinana kwa kutokaa ofisini na badala yake afanye kazi kwa vitendo ili naye aache utumishi uliotukuka.

Baadhi ya viongozi wa dini waliozungumza na gazeti hili, walisema kuwa kuteuliwa kwa Dk Bashiru kumetokana na kazi nzuri ya Tume aliyoiongoza ya kuhakiki mali za CCM. Shehe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Musa Salum alisema Bashiru ni mwadilifu, mchapakazi, mzalendo, mweledi na mpambanaji dhidi ya ufisadi.

Pia, alisema Dk Bashiru alionesha uwezo mkubwa alipokabidhiwa jukumu la kuongoza Tume ya kuhakiki mali za Chama.

Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Methodius Kilaini, alisema kwa kuwa CCM imekuja na msukumo mpya, lazima pia ipate watu sahihi wa kutekeleza msumo huo mpya.

Alisema kuwa Dk Bashiru amepewa jukumu la kuzishughulikia changamoto za Chama, alizozibaini akiwa nje na kuhakikisha kuwa CCM haianguki kutokana na changamoto hizo.
Msekwa, Kafulila, Baregu waguswa uteuzi wa Bashiru Msekwa, Kafulila, Baregu waguswa uteuzi wa Bashiru Reviewed by Zero Degree on 5/31/2018 10:29:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.