Loading...

Yondani, Malima wafungiwa, Chirwa aonywa


BEKI wa Yanga, Kelvin Yondani na mchezaji wa Mbeya City, Ramadhan Malima wamefungiwa na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa ligi kucheza mechi za Ligi Kuu hadi kesi inayowakabili itakaposikilizwa na Kamati ya Nidhamu.

Kosa la Yondani ni kitendo cha kumtemea mate mchezaji wa Simba, Asante Kwasi katika mchezo uliopita dhidi ya watani zao wa jadi, Simba uliochezwa kwenye Uwanja wa taifa, Dar es Salaam na Yanga kufungwa bao 1-0.

Akizungumzia adhabu hizo Mkurugenzi wa Bodi ya Ligi, Boniface Wambura alisema, “waamuzi hawakuona lile tukio ndio maana suala lake limepelekwa kwenye Kamati ya Maadili, na adhabu ya kusimamishwa imetolewa kwa kuzingatia kanuni ya 9(5) ya Ligi Kuu usimamizi wa ligi”.

Kuhusu Malima alisema pia, suala lake limepelekwa kwenye kamati hiyo ya nidhamu. Kosa la mchezaji huyo alitolewa nje kwa kadi nyekundu, lakini akatoka kwenye chumba cha kuvalia nguo kwenda kushangilia bao la kusawazisha la timu yake.

Kwa upande wa Obrey Chirwa wa Yanga alionywa kwa kadi ya njano kwa kosa la kumsukuma mchezaji wa Mbeya City ingawa kwenye picha za televisheni inaonekana kama alipiga kiwiko hivyo, kamati hiyo haikutoa adhabu nyingine kwa vile tayari ameadhibiwa.

“Klabu ya Yanga imeandikiwa barua kuhusu kumuonya mchezaji huyo kwa vile kumbukumbu zinaonesha ameshafanya matukio ya utovu wa nidhamu mara kadhaa akiwa uwanjani,” alisema.

Pamoja na hilo, pia Mkuu wa Habari na Mawasiliano wa klabu ya Simba, Haji Manara amepewa Onyo Kali kwa kuingia uwanjani kushangilia ushindi wa timu yake baada ya mchezo kumalizika.

Wambura alisema kitendo chake ni ukiukwaji wa Kanuni ya 14(11) ya Ligi Kuu kuhusu taratibu za mchezo, na adhabu dhidi yake imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 14(49) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Yondani, Malima wafungiwa, Chirwa aonywa Yondani, Malima wafungiwa, Chirwa aonywa Reviewed by Zero Degree on 5/05/2018 10:08:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.