Loading...

Watendaji CCM wapigwa marufuku kufanya siasa za majukwaani


KATIBU Mkuu mpya wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Bashiru Ally (pichani) amepiga marufuku kwa watendaji wa chama hicho, kufanya siasa za majukwaani kwa kuwa kazi hiyo ni ya Mwenyekiti.

Alisema kuwa viongozi waliochaguliwa kwa miaka mitano mitano, akiwemo Mwenyekiti wa Taifa wa chama akisaidiwa na Makamu wake wawili, Wenyeviti wa CCM wa Mikoa na Wilaya, Wabunge na Madiwani, ndio waliopewa dhamana ya kufanya siasa za majukwaani. Dk Bashiru alisema hayo jana baada ya kukabidhiwa Ofisi ya Katibu Mkuu na mtangulizi wake, Katibu Mkuu mstaafu, Abdulrahman Kinana, kwenye ofisi ndogo za CCM zilizopo Lumumba jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Dk Bashiru, yeye kama Mtendaji, ana wajibu wa kubuni mikakati ya kutekeleza maamuzi ya vikao, kutoa taarifa kwenye vikao, kusimamia maelekezo ya chama, mambo ambayo aliyaita kuwa ni masuala ya mezani na siyo ya jukwaani. “Kama mtendaji, hamtaniona kwenye majukwaa kwa sababu wapo waliopewa dhamana ya kuwa majukwaani; sisi ni watendaji tumeteuliwa, naweza nikakaa nusu saa, saa moja au mwaka mmoja, na ni marufuku kwa mtendaji kufanya kazi ya mwanasiasa,” alisisitiza Dk Bashiru.

Kuhusu mabadiliko ya katiba, alisema atakuwa na msimamo tofauti na ule aliokuwa nao mwanzo. Alisema awali alikuwa huru kutetea mabadiliko ya katiba, lakini kwa kuwa sasa ameingia kwenye siasa za CCM, hana budi kuendana na maelekezo ya chama. “Nazungumza leo kama Katibu Mkuu, ukiwa mchambuzi unachambua hasa; lakini ukiwa msemaji wa chama, unawasilisha yale yaliyoamuliwa kwenye vikao, hivyo kwa sasa siwezi kuchambua yale ambayo hayajaamuliwa na vikao,” alieleza Dk Bashiru.

Kwa upande wake, Kinana alisema alikuwa na majukumu makuu matatu hiyo jana, kwanza kumpongeza Dk Bashiru kwa kuteuliwa na Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Rais John Magufuli na kisha kuchaguliwa na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC). Majukumu mengine ni kumkabidhi ofisi Katibu Mkuu mpya pamoja na makabrasha yote yanayohusu ofisi hiyo; lakini pia alikuwa na jukumu la kumtambulisha kwa watendaji, kazi zilivyokuwa zinafanyika kwenye chama kwa upande wa watendaji na kuwataka watendaji hao wampe ushirikiano kama walivyompa yeye.

Aidha, Kinana aliviomba vyombo vya habari, kumpa ushirikiano Dk Bashiru katika kutimiza wajibu wake huo mpya. Wakati akimkabidhi makabrasha hayo, Kinana alimweleza kwamba yuko tayari kumsaidia, pale atakapohitaji msaada wake. Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Rais mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, alimpongeza Dk Bashiru na kumtakia kila la heri katika majukumu yake hayo mapya. Kikwete pia alimpongeza Katibu Mkuu mstaafu, Kinana, kwa kazi nzuri aliyoifanya kwa chama na kusema kuwa atakumbukwa daima.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Samwel Kiboye, alipongeza uteuzi wa Dk Bashiru na kuwataka wanachama wa CCM nchini kote, kumpa ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yake mapya ndani ya chama. Kiboye alisema hayo alipokuwa akizungumza na gazeti hili jana juu ya hatua iliyochukuliwa na CCM kupitia vikao vyake vya kikatiba, kumteua Dk Bashiru Ally kukiongoza chama kwa nafasi ya ukatibu mkuu. Katika hatua nyingine, Kiboye aliwanyooshea kidole baadhi ya watu ambao hawaungi mkono juhudi zinazofanywa na Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Rais Magufuli katika kuwatumikia wananchi.

Alisema watu wa aina hiyo, hawana uzalendo na mapenzi ya nchi yao. “Nawaomba watanzania na wana CCM wote tumuunge mkono Rais wetu, kwani anafanya kazi kubwa ya kukitumikia Chama na watanzania wote”, alisema. Aliongeza kuwa CCM Mkoa wa Mara, iko pamoja na uongozi wa taifa wa CCM katika utekelezaji wa ilani yake.

Katibu Mkuu huyo mpya wa CCM, aliwasili kwenye ofisi ndogo za chama saa 3:50 asubuhi na kulakiwa na watendaji wa CCM ofisini hapo. Baada ya kukabidhiwa ofisi, Dk Bashiru, Kinana na viongozi wengine, walizungumza na watendaji wa chama hicho kwenye mkutano wa ndani, ambao waandishi wa habari hawakuruhusiwa. Jumanne wiki hii, Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), ilimteua Dk Bashiru kuwa Katibu Mkuu wa CCM baada ya Kinana kujiuzulu wadhifa huo.

Source: Habari Leo
Watendaji CCM wapigwa marufuku kufanya siasa za majukwaani Watendaji CCM wapigwa marufuku kufanya siasa za majukwaani Reviewed by Zero Degree on 6/01/2018 12:20:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.