Maria Nyerere amtaja Dkt Bashiru Ally
Mjane wa Baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere amempongeza Katibu Mkuu wa CCM, Bashiru Ally akimtaka aendelee kuchapa kazi ili kurejesha misingi ya chama hicho.
Taarifa iliyotolewa leo na Idara ya Itikadi na Uenezi ya CCM inaeleza kuwa, Mama Maria amesema Dk Bashiru amekuwa na mchango mkubwa kusaidia utekelezaji wa majukumu ya Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli.
Mama Maria ametoa kauli hiyo baada ya kukutana na Dk Bashiru. Amesema katibu mkuu huyo anakirejesha chama tawala na Serikali katika misingi iliyosimamiwa na Mwalimu Julius Nyerere.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa, kupitia kwa Dk Bashiru, Mama Maria amempongeza Rais John Magufuli kwa kazi nzuri ya ujenzi wa vituo vya afya zaidi ya 200 kote nchini ndani ya kipindi kifupi cha miaka miwili.
“Mama Maria ameeleza vituo hivyo vitakuwa mkombozi wa upatikanaji wa huduma za afya hasa kwa mama, watoto na wazee,” imeeleza taarifa hiyo ikimnukuu mama Maria.
Imeeleza kuwa Mamam Maria ametoa wito kwa CCM kuendelea kuisimamia Serikali na kuimarisha lishe bora kwa watoto, watu wazima na umma ili kujenga Taifa imara.
Dk Bashiru ametumia nafasi hiyo kumshukuru Mama Maria kutokana na kuendelea kujali, kukumbusha na kushauri chama hicho kila anapopata nafasi.
Chanzo: Mwananchi
Maria Nyerere amtaja Dkt Bashiru Ally
Reviewed by Zero Degree
on
12/09/2018 07:50:00 AM
Rating: