Loading...

Guterres asifu mafanikio ya Afrika


Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameuhutubia mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika ambapo amesifu mafanikio katika chaguzi za hivi karibuni, mikataba ya amani na jinsi Afrika inavyowashughulikia wakimbizi.

Wakati wa hotuba yake iliyojaa matumaini Guterres aliunga mkono juhudi za bara la Afrika katika kuifungua mipaka na milango yake na kuonesha mshikamano wa hali ya juu katika kuwasaidia wakimbizi.

Gutteres aliwaambia viongozi wa Afrika na wanadiplomisia wa ngazi ya juu wanaohudhuria mkutano huo kuwa katika juhudi za kutafuta suluhisho la kudumu kwa tatizo la wakimbizi bara la Afrika limekuwa kielelezo cha maana kwa ulimwengu na kwa chombo anachokiongoza.

Kuhusu Afrika inavyojitoa katika kusaidia suala la wakimbizi Guterres amesema "Licha ya changamoto binafsi za kijamii, kiuchumi na kiusalama, serikali za afrika na watu wake zimefungua mipaka, milango na mioyo yao kwa mamilioni ya watu wenye uhitaji.”

Afrika ndiyo inahifadhi zaidi ya theluthi ya wakimbizi na watu walioyahama maskani yao kote ulimwenguni.

Katibu mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesifu pia juhudi za kusaka amani katika mataifa ya Sudan Kusini na Jamhuri ya Afrika ya Kati pamoja ya kuyapongeza mataifa ya Mali, Madagascar na DR Congo ambayo yalifanya uchaguzi hivi karibuni.

Guterres alifumbia macho baadhi ya kasoro?

Hata hivyo Guterres hakutaja hatari ambazo wakimbizi na watu waliopoteza makazi wanakabiliana nazo katika nchi za Afrika na lawama zilizogubika chaguzi zilizofanyika barani humo.

Kulingana na Umoja wa Mataifa wahamiaji na wakimbizi katika nchi kama Libya wamekuwa wakikabiliana na visa vya unyanyasaji, kufanyishwa kazi kwa nguvu na kufungwa jela.

Kadhalika Matokeo ya uchaguzi katika Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo yalizozaniwa kutokana na madai ya wizi wa kura na ukiukwaji wa taratibu za kupiga kura.

Zaidi ya wapiga kura milioni moja hawakushiriki uchaguzi huo kwa sababu za mlipuko wa maradhi ya Ebola na mapigano ya makundi yenye silaha katika maeneo kadhaa nchini Congo.

Nchini Madagascar upande wa upinzani ulilalamikia matokeo ya uchaguzi kwa kile ilichosema tarabibu za uchaguzi zilipindishwa.

Guterres alishindwa vile vile kuuzungumzia uchaguzi wa mwaka jana nchini Zimbabwe ambao watu sita waliuwawa na vikosi vya usalama.

Al- Sissi amrithi Kagame uenyekiti wa AU

Katika hatua nyingine mkutano huo wa kilele umeshuhudia rais wa Rwanda Paul Kagame ambaye aliongoza juhudi za mageuzi ya Umoja wa Afrika akikabidhi wadhifa wa uenyekiti wa kupokezana wa umoja huo kwa rais wa Misri Abdel-Fattah al-Sissi.

Al-Sissi ambaye atakuwa mwenyekiti kwa kipindi cha mwaka mmoja ametangaza kuwa suala la usalama ndilo litakalokuwa ajenda ya kipaumbele wakati wa muhula wake.

Mbali ya kujadili mizozo kadhaa inayoendelea barani humo, mkutano huo utaangazia pia masuala ya mageuzi ya Umoja wa Afrika ikiwemo ajenda ya uanzishwaji wa kanda huru ya kibiashara ya bara zima.

Itifati ya kuanzisha kanda huru ya kibiashara barani Afrika ilikubaliwa na mataifa 44 mwaka 2018 lakini imeshindwa kuanza kufanya kazi kwa kuwa ni mataifa 19 pekee yaliyoiidhinisha badala ya 22 yanayohitajika.

Chanzo: Dw
Guterres asifu mafanikio ya Afrika Guterres asifu mafanikio ya Afrika Reviewed by Zero Degree on 2/11/2019 12:05:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.