TP Mazembe yaibeba Yanga CAF
YANGA wamezidi kupata mteremko kuelekea mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zesco utakaochezwa kesho kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, baada ya TP Mazembe ya DR Congo kutia mkono wao.
Wakati Zesco wakiingia kimya kimya nchini, tayari Yanga wamemaliza kazi baada ya kukusanya kila kitu kitakachowawezesha kuwapiga mabao mengi Wazambia hao, kuanzia mbinu zao na wachezaji hatari wa kuchungwa katika mchezo huo.
Licha ya Wanajangwani hao kuisoma timu hiyo kupitia video za michezo mbalimbali waliyocheza, TP Mazembe nao wameamua kutia mkono kuhakikisha Zesco hawatoki salama kwenye Dimba la Taifa.
Ishu yenyewe iko hivi, baada ya Wacongo hao (Mazembe) kufahamu kuwa ndugu yao, Mwinyi Zahera, anatarajia kukabiliana na Zesco, Kocha Mkuu wa vigogo hao wa soka Afrika, Mihayo Kazembe, amemtumia video ya mechi waliyocheza nao, kisha kumweleza mambo kadhaa ya vitu anavyotakiwa kufanyia kazi kiufundi.
TP Mazembe walikutana na Zesco katika raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita na kufanikiwa kuitoa baada ya kuifunga bao 1-0 nyumbani na kutoka sare ya 1-1 nchini Zambia.
Kulingana na taarifa ya Bingwa, Zahera alisema hana kitu asichokijua juu ya wapinzani wake hao, akisubiri kukutana nao uwanjani tu ili awamalize.
Zahera alisema Zesco ni timu inayocheza michuano ya Afrika karibia kila msimu, lakini hilo halimpi presha kwani kazi ameshamaliza na anajua kitu gani anatakiwa kufanya kulingana na taarifa alizozipata.
“Zesco kila kitu chao ninacho, tumeangalia video zao za michezo ya zamani na hivi karibuni, kizuri zaidi kocha wa TP Mazembe amenitumia video ya mechi yao na kuniambia baadhi ya vitu vya kufanya.
“Kutokana na hilo sina wasiwasi, ukiangalia mazoezi tunaendelea na kufanya na wachezaji wana morali na wamekaa katika mstari ninaotaka, kama ni ndege imetua pale pale ninapotaka,” alisema Zahera.
TP Mazembe yaibeba Yanga CAF
Reviewed by Zero Degree
on
9/13/2019 07:00:00 AM
Rating:
