Loading...

Utetezi wa Lissu wagonga mwamba


Mahakama Kuu nchini Tanzania imekataa maombi ya aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki kwa tiketi ya Chadema,Tundu Lissu kuhusu kutengua uamuzi wa Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai uliofuta ubunge.

Mahakama kuu imesema mwanasheria mkuu huyo wa Chadema hakupaswa kuwasilisha maombi hayo, alitakiwa kufungua kesi ya kupinga uchaguzi wa ubunge katika jimbo hilo.

Akisoma uamuzi huo wa mahakama, Jaji Sirillius Matupa amesema kama maombi yake yakikubaliwa yatasababisha uvunjaji wa katiba kwa kuwa italazimika kuwa na wabunge wawili kwenye jimbo moja.

Lissu alifungua maombi chini ya hati ya dharura, kupitia kwa kaka yake Alute Mughwai ambaye amempa mamlaka ya kisheria kumuwakilisha, ikiwa ni hatua ya awali kabisa ya kupigania kurudishiwa ubunge wake.

Katika maombi hayo namba 18 ya mwaka 2019, dhidi ya Spika wa Bunge na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Lissu aliomba kibali cha kufungua shauri kupinga taarifa ya Spika ya kukoma kwa ubunge wake.

Mwanasiasa wa upinzani nchini Tanzania Tundu Lissu alitangaza kupinga kupinga mahakamani uamuzi wa kumuondolea sifa ya ubunge kwa kile alichodai kuwa ni kinyume cha sheria.

Katika waraka wa salamu alizozitoa kwa marafiki zake, Lissu alisema tangu alipopoteza ubunge, "sijasema maneno mengi sana, zaidi ya kusema kwamba tutaenda Mahakama Kuu kupinga uamuzi huo."

"Kesi za ubunge, kama zilivyo kesi zote za uchaguzi wa kisiasa, ni kesi za kisiasa. Ni mwendelezo wa mapambano ya kisiasa katika uwanja tofauti. Kwa sababu hiyo, ni kesi nyeti na za kipekee sana. Zinahitaji umakini mkubwa katika kuziandaa na kuziendesha. Nina uzoefu mkubwa nazo, kwa sababu nimezifanya sana tangu 2005."

Juni 28, 2019 Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai alilieleza bunge kuwa Lissu amepoteza sifa ya ubunge kwa sababu mbili, mkiwemo kutokujaza fomu za mali na madeni kwa viongozi wa umma na kutotoa taarifa ya wapi alipo.

Mawakili wa Lissu walitarajia kuzuia kuapishwa kwa Mtaturu mpaka kesi hiyo itakaposikilizwa na kuamuliwa.

Hata hivyo, Jaji Sirillius Matupa alilikataa ombi hilo la mawakili wa Lissu akisema katika kesi za ubunge hata kama mtu ameapishwa anaweza kuvuliwa ubunge pamoja na kiapo chake.

Uamuzi huo umewasikitisha wanachama wa Chadema, huku mwenyekiti wake na Kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni Freeman Mbowe amesema bado wataendelea kupigania haki hiyo.

''Mahakama ni chombo tunachokiheshimu kama chama, sote tumesikia maamuzi ya jaji katika kesi iliyokuwa katika mahakama kuu siku ya leo, ndugu yetu Lissu bado yuko nje kwa matibabu na tutafanya mawasiliano katika chama na tutaendelea kuitafuta haki hii. Tunatambua haki hii haiwezi kupatikana kwa urahisi kutokana na sababu mbalimbali katika mahakama kuna ngazi mbalimbali za kupata haki hiyo kwa hiyo tutaendelea kutumia kila mfumo wa kimahakama kuhakikisha kuwa haki hiyo inaendelea kupiganiwa na kutafutwa.Tutarejea katika mahakama hii kwa utaratibu ambao tutashauriana na kukubaliana''. Alisema Mbowe.

Lissu alifungua maombi chini ya hati ya dharura, kupitia kwa kaka yake Alute Mughwai, ambaye alimpa mamlaka ya kisheria kufanya hivyo, akitaka kurudishiwa ubunge wake.

Lissu anapinga vikali kuvuliwa wadhifa wake akidai kuwa amefutwa ubunge huku ikifahamika wazi kuwa amekuwa nje kwa matibabu tangu tarehe 7 mwezi Septemba mwaka 2017, baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana.

Mwanasiasa huyo aliiambia BBC kuwa alitarajia hatua zilizochukuliwa na Spika dhidi yake kwa sababu alishasema kwa hiyo ilipotokea mwezi wa sita wala haikuwa ajabu.

''Mtu ambaye alishakuwa na nia ya kunifuta ubunge nisingeweza kumzuia, vinginevyo labda ningesema niachane na habari ya matibabu nirudi Tanzania''.
Utetezi wa Lissu wagonga mwamba Utetezi wa Lissu wagonga mwamba Reviewed by Zero Degree on 9/09/2019 06:20:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.