Loading...

Bodi ya Ligi kushughulika na washirikina msimu ujao

Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Steven Mguto

Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara imesema kuelekea msimu ujao itatengeneza kanuni ya kuzikata pointi timu zitakazofanya au kuonyesha imani za kishirikina viwanjani wakati wa mchezo.

Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Steven Mguto, alisema wao kama bodi, Shirikisho la Soka Nchini (TFF) na wadau wengine wa soka, wanataka kutengeneza kanuni ya kuzikata pointi timu kutokana na kukithiri kwa vitendo hivyo msimu huu, akisema faini peke yake hazitoshi.

"Tutaweka sheria kali ambazo klabu zitaogopa na hazitafanya vitu kama hivi vya makusudi, moja ya sheria ni adhabu ya kunyang'anywa pointi, tukiweka hii watu watatia akili, hawatafanya mambo ya ovyo ovyo," alisema Mguto.

Amesema moja ya mambo yaliyowasumbua sana msimu huu ni matukio ya imani za kishirikina na wamezipiga sana faini klabu, lakini bado zinaonekana kutowaathiri wahusika.

"Wala isidhaniwe kuwa sisi tunapenda kuwapiga faini ili tupate fedha, sisi faini siyo bajeti yetu ya kujiendesha, lakini tunawajibika kufanya hivyo, naona bado haziwafundishi, tutakuja na sheria nyingine msimu ujao.

Sasa naona tukianza kuwakata pointi labda itasaidia kuondoa vitendo hivi," alisema Mguto.

Msimu uliomalizika jana, kulikuwa na matukio mengi ya vitendo mbalimbali ambavyo kwa mujibu wa bodi hiyo, vilikuwa vinaashiria ushirikina.

Klabu mbalimbali, zikiwamo za Simba na Yanga mara kwa mara zimekuwa zikikutana na adhabu za kutozwa faini.
Bodi ya Ligi kushughulika na washirikina msimu ujao Bodi ya Ligi kushughulika na washirikina msimu ujao Reviewed by Zero Degree on 5/29/2024 04:30:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.