Loading...

Benchikha bado yupo sana Simba

Kocha wa Simba SC, Abdelhak Benchikha.

WAKATI leo akikiongoza kikosi chake kuivaa KVZ FC kwenye mechi ya Kombe la Muungano, Klabu ya Simba imesema haina mpango wowote wa kuachana na kocha wao, Abdelhak Benchikha, kama inavyoanza kuvumishwa na baadhi ya watu, huku ikiweka wazi kuwa tayari imeshakutana naye kwa ajili ya kujadili tathimini ya maboresho ya kikosi cha timu hiyo kwa msimu ujao wa mashindano.

Kauli hiyo inakuja baada ya kuwapo kwa taarifa katika mitandao mbalimbali na baadhi ya wachambuzi wa soka juu ya kocha huyo, wakidai yupo hatarini kutupiwa virago kuondoka ndani ya timu hiyo baada ya matokeo mabovu.

Akizungumza na Nipashe jana, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema hakuna ukweli juu ya nia yoyote au mpango wa kumtimua au kusitisha mkataba na Benchikha kwani ni kocha mkubwa Afrika na wanamuamini.

Aliwataka mashabiki kutulia kwa kipindi hiki cha mpito na kuimarisha nguvu na mshikamano kwa ajili ya kuimarisha timu yao kwa msimu ujao kulingana na mapendekezo ya benchi la ufundi linaloongozwa na Benchikha.

“Hatuna mpango huo wa kumuondoa au kuachana na Benchikha, Wanasimba wanatakiwa kupuuza taarifa zilizosambaa kuhusu kocha wetu, bado yupo kwenye mipango ya klabu na sasa wazo na mikakati yetu ni kuboresha na kujenga timu ya msimu ujao, lakini pia kuhakikisha tunafanya vizuri katika michezo iliyopo mbele yetu.

"Benchikha yupo sana na leo (jana) mchana alikuwa sehemu ya timu iliyoenda visiwani Zanzibar kwa ajili ya michuano ya Kombe la Muungano ikiwa ni sehemu ya mipango ya kuhakikisha tunafanikiwa kushinda kombe hilo,” alisema Ahmed.

Aliongeza kuwa kikosi kipo vizuri na wachezaji wote wako salama na wako kwenye msafara huo kasoro wawili, beki Shamari Kapombe, aliyeumia kwenye mazoezi ya kujianda na michezo ya Kombe la Muungano.

Ahmed alisema mchezaji mwingine ambaye hajaambatana na timu ni kiungo Sadio Kanoute mwenye majeraha baada ya kuumia kwenye mchezo wa dhidi ya Yanga wikiendi iliyopita.

Alisema wachezaji wapo tayari kwa ajili ya michuano hiyo ya Kombe la Muungano kwa kufanya vizuri katika mchezo wa kwanza wa nusu fainali dhidi ya KVZ FC ya visiwani humo.

Simba leo saa 2:15 usiku inamenyana na wenyeji, KVZ katika Nusu fainali ya Kombe la Muungano, itakayopigwa Uwanja wa New Amaan Complex visiwani, Zanzíbar wakati Azam FC Alhamisi itavaava na KMKM, na Washindi wa mechi za hizo za watakutana katika fainali ya michuano hiyo Aprili 27, mwaka huu uwanjani hapo.

Chanzo: Nipashe
Benchikha bado yupo sana Simba Benchikha bado yupo sana Simba Reviewed by Zero Degree on 4/24/2024 01:23:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.