Loading...

Spika wa Bunge Afrika Kusini ajiuzulu



CAPE TOWN, Afrika Kusini: NOSIVIWE Mapisa-Nqakula amejiuzulu rasmi nafasi ya uspika wa Bunge la Afrika Kusini kutokana na tuhuma za ufisadi.

Katika barua yake ya kujiuzulu ya Aprili 3, Mapisa-Nqakula ameandika kujiuzulu nafasi ya Spika wa Bunge na Mbunge, ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zilizotolewa dhidi yake.

“Kujiuzulu kwangu sio dalili wala kukiri kuwa na hatia kuhusiana na tuhuma zinazotolewa dhidi yangu, nimefanya uamuzi kwa ajili ya kudumisha uadilifu na utakatifu wa bunge letu ambalo ni taasisi kuu ya mfumo wetu wa serikali inayowakilisha Waafrika Kusini,” amesema Mapisa.

Kujiuzulu kunakuja baada ya Mahakama Kuu ya Gauteng huko Pretoria kutupilia mbali rufaa yake ya dharura ya kuzuia Mamlaka ya Kitaifa ya Mashtaka (NPA) na Huduma ya Polisi ya Afrika Kusini kumkamata kwa tuhuma za rushwa.

Shirika la Utangazaji la Serikali ya Afrika Kusini SABC, liliripoti kwamba anashukiwa kupokea mamilioni ya pesa taslimu kama hongo kutoka kwa mkandarasi wa zamani wa kijeshi katika kipindi chake cha Uwaziri wa Ulinzi. Mapisa-Nqakula alikuwa Waziri wa Ulinzi kutoka mwaka 2012 hadi 2021.

Jumanne, News24 iliripoti kwamba Mahakama Kuu ya Gauteng huko Pretoria ilipinga ombi la pili la dharura la Mapisa-Nqakula la kuizuia serikali kumkamata kwa tuhuma za ufisadi. Uamuzi huo ulifungua njia kwa Serikali kumkamata Mapisa-Nqakula na kumfikisha mahakamani.

Rushwa hizo zinadaiwa kulipwa baada ya aliyekuwa mhudumu hewa na mfanyabiashara Nombasa Ntsondwa-Ndhlovu, ambaye ni mkurugenzi pekee wa Umkhombe Marine (Pty) Ltd na yeye mwenyewe mtuhumiwa wa utapeli wa zabuni kupokea malipo ya mikataba ya utetezi aliyopokea.

Katika barua yake, Mapisa-Nqakula amesema: katika kanuni “kila Mwafrika Kusini ahesabiwe kuwa hana hatia hadi itakapothibitishwa kuwa na hatia”.

“Kutokana na imani ya umma iliyonikabidhi kama Spika wa Bunge letu na hitaji la mimi kulinda taswira ya chama chetu, African National Congress, nina wajibu, licha ya kanuni kwamba nionekane sina hatia, nachukua hatua ya kujiuzulu,” amesema Mapisa huku akidai ataendelea kuwa mwanachama wa ANC.

ANC ilithibitisha kwamba Katibu Mkuu Fikile Mbalula amepokea barua ya kujiuzulu ya Mapisa-Nqakula.

Naye msemaji wa ofisi ya Bunge la Afrika Kusini, Moloto Mothapo amesema Spika wa Bunge hilo anamshukuru Mapisa-Nqakula kwa utumishi wake.

“Kaimu Spika wa Bunge anatoa shukurani kwa Mapisa-Nqakula kwa utumishi wake kwa taifa katika kipindi chake cha miaka 30 kama Mbunge na hivi majuzi katika nafasi ya Spika wa Bunge tangu tarehe 19 Agosti 2021 ,” Mothapo ameeleza.

Chanzo: Habari leo
Spika wa Bunge Afrika Kusini ajiuzulu Spika wa Bunge Afrika Kusini ajiuzulu Reviewed by Zero Degree on 4/04/2024 09:47:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.