Loading...

Uchaguzi 2025: Msuya amtahadharisha Rais Samia

Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais mstaafu, Cleopa David Msuya

WAZIRI Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais mstaafu, Cleopa David Msuya, amepongeza utendaji kazi wa Rais Samia Suluhu Hassani katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati iliyoachwa na mtangulizi wake, huku akitoa tahadhari kwa watu wanaomzunguka rais, akidai wanaweza kuwa kikwazo katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Wakati akitoa tahadhari hiyo amesema Watanzania wanapashwa kujivunia Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, na kwamba kinachotakiwa kwa serikali zote ni kuendelea kujenga mifumo ya kuelimisha wananchi wa pande zote mbili ili uendelee kuwa na faida zaidi kwa wananchi.

Msuya amesema hayo leo Jumamosi Aprili 6, wakati akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake Upanga jijini Dar es Saalam, kuhusu miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

“Nilipata kuonana naye siku moja (Rais Samia Suhuhu Hassani) nikamwambia mama tatizo lako kwenye uchaguzi ujao halitakuwa huko chini labda tatizo lako litakuwa kwa hao watu wanaokuzunguka, maana jina likipita kwenye CCM kule chini watakupitisha tu,” amesema.

Msuya amesema Rais Samia anaendesha mambo haya kwa nia nzuri na kwamba Tanzania inajivunia licha ya mapungufu madogo ambayo yamejitokeza hapa katikati (japo hakuyataja), lakini akasema Tanzania ni nchi ambayo inatawaliwa kisheria na katiba yake inaheshimika.

“Watu wote wa nje na wa ndani wanakubali hilo, kila mmoja anafahamu jinsi mzee Mwinyi (Rais Ali Hassan Mwinyi), alivyopatikana na alivyochaguliwa kuwa rais, lakini hivi karibuni baada ya kifo cha Magufuli (Hayati Dk. John Magufuli) ‘automaticaly’ naibu wake (Makamu wa Rais), ambaye alikuwa Mama Samia ndio akachukua mamlaka bila mtikisiko wowote, ingekuwa nchi nyingine ni vita, na hasa kama ni mama lakini taratibu zikafuatwa akaapishwa kuwa rais na yeye akamchagua makamu wa rais,” amesema.

Msuya amesema ana matumaini makubwa na Rais Samia na kwamba kuna vitu fulani amefanikiwa sana kuvifanya.

“Alipochukua kapu kuna kauli mbili alizitoa, ya kwanza alisema mnayemuona hapa ni rais wa Jamhuri ya Muungano sio mama, kwa maneno mengine rais ni ‘institution’ (taasisi) ambayo anayo, sawa na zile zile walizokuwa nazo wengine wote waliomtangualia,” amesema.

Amesema alitoa kauli hiyo ili watu wajue kwamba hakuna mtu legelege pale juu.

Kauli ya pili kwa mujibu wa Msuya, ni pale Rais Samia aliposema yale aliyoanza na mwenzake (Dk. Magufuli), yaani miradi ya kimkakati atajitahidi aiendeleze na kuongeza mingine kila atakapoona inafaa.

Mtazamo wake juu ya awamu sita za uongozi alizoshuhudia

Kiongozi huyo amepongeza awamu zote sita za uongozi ambao kwa asilimia kubwa wamepambana kuhakikisha kuwa wanalinda katiba na maslahi ya wananchi.

“Miongoni wa vitu ambavyo Watanzania wangejivunia ni kwamba pamoja na changamoto ambazo zimejitokeza hapa na pale, Tanzania ni nchi ambayo inatawalia na misingi ya kisheria na katiba yake inaheshimika. Mtu yeyote wa ndani na nje anakubaliana na hilo,” amesema na kuongeza;

“Kwa mfano mzee Mwinyi alipochaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano badala ya Nyerere na hata hivi karibuni baada ya kifo cha Rais Magufuli, naibu wake Rais Samia alichaguliwa kuwa Rais bila mtikisiko wowote tofauti na nchi nyingine ambapo tungeweza kushuhudia vita."

Kwa mujibu wake licha ya katiba kuheshimu utaratibu uliotumikika kumuweka madarakani Rais Samia, yeye pia (Samia) kwa namna moja ama nyingine aliheshimu katiba katika kuteua Makamu wa Rais pamoja na Waziri Mkuu.

Akizungumzia uongozi wa Rais Samia amesema kwa asilimia kubwa umekuwa ni wa mafanikio na ameonesha ujasiri mkubwa wa kuendeleza pale alipoishia Rais Magufuli.

Kwa mujibu wa Msuya, uongozi wa Rais Samia umekuwa na mafaniko makubwa akiainisha kauli yake ‘Aliyesimama hapa ni Rais Mwanamke’ aliyoitoa wakati wa msiba wa aliyekuwa Rais Magufuli, ambayo Rais Samia alitaka kuonesha kwamba Rais ni Taasisi, na mamlaka aliyonayo ndio waliyokuwa nayo viongozi wengine waliopita.

Kwa upande wa pili amesema kauli hiyo ililenga kuonesha kuwa hakuna mtu legelege juu na kwa upande mwingine kuonesha kuwa alikuwa tayari kumaliza miradi ya kimkakati waliyoanza na Rais Magufuli.

“Nilipata kuonana naye siku moja nikamuambia kwamba mama nafikiri tatizo lako uchaguzi ujao, halitakuwa huko chini, labda tatizo lako litokee kwa hawa watu waliokuzunguka hapo maana kama jina likipita kwenye CCM pale kule chini watapitisha tu. Kwahiyo mtazamo wangu ni kwamba ameendesha nchi kwa nia nzuri na amejitahidi kufanya watu wamuelewe na kwamba dalili zinaonesha kuwa mambo yataenda sawa,”

Muungano

Rai kubwa aliyoitoa kiongozi huyo ni kwamba ni muda wananchi walichukulie suala la muungano chanya, badala ya kuleta hoja zisizo za msingi.

Amefananisha suala la muungano na ndoa na kueleza kuwa muungano wowote haukosi changamoto na lazima yatafutwe majibu ya kukabiiana nazo.

“Muungano ni kitu kizuri. Unapoanza safari, kunakuwa na matatizo. Ni muda wananchi wajivunie kurithi muungano ambao wengine wameshindwa kuuendeleza," amesema na kuongeza.

“Maana ya kuungana ni kupunguza gharama na kuongeza ufanisi. Maneno, changamoto zipo. Picha kubwa ni kwamba mafanikio yapo kwa sababu ya kuheshimu ya misingi ya mfumo."

Kwa mujibu wake asilimia kubwa ya watu wanaobeza kuwepo kwa muungano hata watapoulizwa matunda wanayoyaona kwa upande wa bara watatoa jibu hilohilo.

“Serikali iweke juhudi za kuhakikisha kuwa wanaelimisha vijana kewa mbinu mbalimbali ili waweze kuelewa tija ya muungano," amesema.

Waziri mkuu mstaafu huyo pia ametoa ufafanuzi kuhusiana na kauli aliyowahi kuitoa katika bunge la bajeti la mwaka 1989 kuwa “Kila mtu abebe msalaba wake” ambayo ilipokewa na hisia tofauti za watanzania.

“Hilo la kusema kwamba kila mtu abebe msalaba wake, ndio nilisema. Sababu yake ni nii? Tumepeleka bajeti hapo bungeni. Shida zetu ni zile zile ambazo mpaka leo Waziri wa fedha anazi-face (anakabiliana nazo). Mapato, msingi wa mapato ya serikali ni mdogo. Kwa hiyo katika bajeti ile tulipandikiza kodi katika kanga, vitenge, pamoja na mambo mengine," amefafanua.

Ameoongeza kusema: “Sasa katika hoja zilizotolewa pale ndani na wabunge wakati wengine wanapinga hilo. Basi oh!! Mimi nina wake wawili nitawezaje kuwavisha wake zangu wote wawili kanga na vitenge kama umepandisha kodi. Kwa kweli nikasema ni unfair kupandisha taifa kodi kwa sababu umeona kuwa na luxury ya kuwa na wake watatu, niseme basi tutakuachia ili wanunulie kanga na vitenge wewe usiguswe. Lakini mimi nilie na mke mmoja niguswe. Kwa hiyo nilijibu hivyo.”

Msuya aliendelea kusema: "Kutoa kauli ile baadhi ya watu waliichukua na kusema kuwa huyu mtu yule hafai kuwa Waziri mbona si mjamaa. Kwanini hataki kutoa vitu sawasawa kwa kila mtu akifikiri kwamba hiyo itaongeza kasi kwa huyo anaeteua mawaziri aamue kuniondoa au kutoniondoa. Mimi nilikuwa huru kabisa kwenye fikra zangu."

Baada ya hapo, Msuya alikutana na Rais: "Lakini bahati nilipokutana na rais nafikiri siku mbili baadae, nafikiri wakati ule alikuwa Mzee Mwinyi akaniambia, Bwana huku serikali kuna kautaratibu, kuna ripoti za siri zinaandikwa na idara ya usalama ambayo kila siku inakwenda kwa Rais, Waziri Mkuu, nafikiri kwa sasa hivi pia inaenda kwa Makamu wa Rais. Ilipofika kwake alisema watu kwenye baa kwenye mabasi wanasema, ‘Eeh, Bwana! Afadhali tumeambiwa ukweli! Watu wanatudanganyadanganya tu. Huyu katuambia ukweli, kama unataka kuoa, nguvu yako. Lakini usiwe mzigo kwa wenzako. Kwa hiyo wakajifuta wenyewe."

Msuya anaendelea kueleza: "Unajua katika haya mambo ya politics ukijaribu kutegemea sana umaarufu na siasa, watanzania ni watu ambao wanafikiri mambo. Mimi nilisema vile kwa nia nzuri lakini mwitikio wake kwenye hizo ripoti za SITREP zikasema response kwa watu wa kawaida kwenye mabasi, kwenye mabaa, kokote huko wanasema afadhali tumeambiwa ukweli bwana! Hawa wengine wanatudanganyadanganya tu. Sasa mnaweza kuamua wenyewe kama ndio hiyo ilinifanya nikabaki pale. Nilikaa hazina kama mara mbili hivi, mara tatu."

Kuhusiana na kuungua kwa benki kuu mwaka 1984, Msuya amesema kuwa ni kweli benki iliungua na kamati iliundwa na kuratibiwa, wazo ambalo lilitolewa na hayati marehemu Samuel Sitta kufanya uchunguzi ambapo ilibainika kuwa tukio hilo halikutokana na nia mbaya wala hujuma bali ilikuwa ni bahati mbaya tu.

Chanzo: Nipashe
Uchaguzi 2025: Msuya amtahadharisha Rais Samia Uchaguzi 2025: Msuya amtahadharisha Rais Samia Reviewed by Zero Degree on 4/07/2024 01:55:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.