Loading...

Feitoto ameonyesha uwezo mkubwa sana - Azizi Ki


Licha ya kuibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu msimu uliomalizika juzi, kiungo wa Yanga amemsifu na kumpongeza nyota wa Azam FC, Feisal Salum 'Feitoto' kwa upinzani mkali aliounyesha kwenye kuwania tuzo hiyo.

Aziz Ki alisema, Fei toto ameonyesha uwezo mkubwa msimu huu akiichezea Azam baada ya kuondoka Yanga na alikuwa mpinzani wa kweli kwenye mbio hizo za kuwania tuzo hiyo ya mfungaji bora msimu huu.

Alisema ameshukuru kumaliza ligi akiwa mfungaji bora na anaamini mabao aliyoyafunga yamechangia kwa timu yake kuchukua ubingwa msimu huu.

Aziz Ki amemaliza ligi akiwa na mabao 21 akimzidi Feitoto mabao mawili baada ya kuchuana kwa muda mrefu lakini mechi za mwisho juzi ziliamua nani wa kutwaa tuzo hiyo.

"Nafurahi nimeisaidia timu yangu kuchukua ubingwa na mimi kumaliza na mabao mengi, nawashukuru wachezaji wenzangu kwa ushirikiano wao, lakini siwezi kuacha kumsifia Feitoto, tulichuana kwa muda mrefu, ni mchezaji mzuri na ameonyesha uwezo mkubwa sana akiwa na timu yake, binafsi namkubali sana," alisema Azizi Ki.

Alisema anampongeza sana Feitoto na ameonysha yeye ni mchezaji mkubwa na mwenye kipaji Tanzania.

Kwa upande wake, Feitoto alimpongeza mchezaji mwenzake huyo wa zamani ndani ya Yanga kwa kumaliza Ligi akiwa mfungaji bora.

"Hongera sana kwake kwa kumaliza akiwa na mabao mengi, namfahamu ni mchezaji mzuri na kwa kile alichokionyesha anastahili pongezi," alisema Feitoto.

Alisema kama mchezaji anafuraha kuona timu yake imefuzu kucheza michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kumaliza katika nafasi ya pili nyuma ya mabingwa, Yanga.

"Lengo la kwanza ilikuwa kuisaidia timu kufuzu kwa michuano Ligi ya Mabingwa Afrika, nashukuru Mungu tumefanikiwa, kukosa tuzo ya kiatu kwangu sio kitu kama tungekosa tiketi ya kushiriki michuano hiyo," alisema Feitoto.
Feitoto ameonyesha uwezo mkubwa sana - Azizi Ki Feitoto ameonyesha uwezo mkubwa sana - Azizi Ki Reviewed by Zero Degree on 5/30/2024 05:22:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.