Loading...

Mpira ni mchezo wa makosa, tumefanya makosa wametuadhibu - Gwalala


Baada ya kukung'utwa mabao 3-0 ugenini dhidi ya Bravos do Maquis ya Angola, wachezaji wa Coastal Union wamesema hali ya hewa iliwaathiri kwa kiasi kikubwa katika mchezo huo.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Gerald Gwalala, alisema hali ya baridi nchini Angola ilichangia kwa kiasi kikubwa, lakini pia matumizi ya nguvu kwa wapinzani wao pia lilikuwa tatizo kwao.

"Mchezo ulikuwa mgumu upande wetu, baadhi ya vitu vilituathiri, kwanza ni hali ya hewa, lakini wenzetu walikuwa wakicheza soka la kutumia mabavu zaidi, ila benchi la ufundi limeona, mpira ni mchezo wa makosa, tumefanya makosa wametuadhibu, naamini makocha watatupa maelekezo kuelekea mechi ya pili nyumbani, mchezo haujaisha mpaka marudiano," alisema Gwalala.

Ulikuwa ni mchezo wa Kombe la Shirikisho barani Afrika, uliopigwa juzi Uwanja wa Nacional da Tundavala nchini Angola, ukiwa ni wa kwanza wa kimataifa kwa wawakilishi hao wa Tanzania baada ya miaka 35. Mara ya mwisho kwa timu hiyo kucheza mechi za kimataifa ilikuwa ni 1989, baada ya kutwaa Ubingwa wa Tanzania Bara 1988.

Yalikuwa ni mabao ya Joaquim Cristovao Paciencia dakika ya 22 na 45 na Luis Manico Goncalves dakika ya 81, yaliyoiweka Coastal kwenye wakati mgumu kwa kusonga mbele kwenye hatua ya raundi ya kwanza ya michuano hiyo, ambapo sasa italazimika kushinda kuanzia mabao 4-0 katika mchezo wa marudiano utakaopigwa, Agosti 25, mwaka huu Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Kocha Mkuu, David Ouma, alionyesha kusikitishwa na timu yake kuruhusu mabao rahisi, mawili yakiwa ya aina moja.

"Dakika 15 za mwanzo tulicheza vema, lakini baadaye tukapotea, tumefungwa mabao ya aina moja, tumeruhusu mabao rahisi sana," aliongea kocha huyo kwa masikitiko.
Mpira ni mchezo wa makosa, tumefanya makosa wametuadhibu - Gwalala Mpira ni mchezo wa makosa, tumefanya makosa wametuadhibu - Gwalala Reviewed by Zero Degree on 8/19/2024 12:10:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.