Loading...

Wauguzi matatani kumuomba rushwa mjamzito


Wahudumu katika Kituo cha Afya cha Ngaya kilichopo katika Halmashauri ya Msalala mkoani Shinyanga wanatuhumiwa kuomba rushwa ya Sh.150,000 kutoka kwa familia ya mama aliyejifungua mtoto kituoni hapo.

Mkono wa mtoto wa mama huyo ulibainika umevunjika, hivyo wahudumu hao walimuomba kiasi hicho cha fedha ili wamtibu.

Madai hayo yametolewa juzi na mama huyo aliyejifungua, Sophia Budeba na kueleza kuwa licha ya kuombwa kiasi hicho cha fedha awali alipofika kituoni hapo aliombwa pia Sh.40,000 kwa ajili ya kupatiwa huduma ya kujifungua.

Sophia alisema baada ya kutoa kiasi hicho Mei, 18 alipatiwa huduma lakini wakati wa kujifungua mtoto alikuwa ametanguliza mabega hali ambayo ilisababisha mkono kuvunjika wakati akizaliwa.

“Baada ya mkono huo wa kulia kuvunjika tuliombwa Sh. 150,000 kwa ajili ya mtoto huyo kufungwa POP na baada ya hapo alipewa rufani Kwenda Hospitali ya Halmashauri,” alisema Sophia.

Muuguzi Mfawidhi wa Hospitali ya Manispaa ya Kahama, Magreth Kiyenze, alikiri mtoto huyo kupatiwa rufani baada ya kugundulika kuvunjika mkono wakati wa kuzaliwa kwa ajili ya matibabu zaidi.

“Matibabu ya watoto wadogo chini ya miaka mitano ni bure na huduma za mama na mtoto wa chini ya miaka mitano zinatolewa bila malipo yeyote,” alisema Kiyenze.

Mganga wa zamu katika wodi namba sita ya watoto wachanga katika Hospitali ya Manispaa kahama, Philipo Laizer alisema walimpokea mtoto wa kiume mwenye uzito wa kilo tatu na nusu kutoka kituoni hapo.

Alisema walipomfanyia uchunguzi waligundua amevunjika mkono wa kulia na kuufunga mkono nusu ili kuupa nguvu.

Aidha, baba wa mtoto huyo, Jumanne Paulo alithibitisha kurejeshewa fedha hizo baada ya kutoa taarifa kwa uongozi ngazi mbalimbali.

Jana, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha alimtembelea mtoto huyo hospitalini ili kumjulia hali na kuthibitisha kuwa suala la rushwa tayari lipo katika mamlaka husika ambayo ni Taasisi ya Kuzua na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Macha alisema: “Yaliyoonekana kwenye kituo hicho cha afya ni mazingira ya rushwa yanayoonekana kwenye maeneo mengine ya kutolea huduma, tutaendelea kupiga vita ili wananchi wapate huduma stahiki”
Wauguzi matatani kumuomba rushwa mjamzito  Wauguzi matatani kumuomba rushwa mjamzito Reviewed by Zero Degree on 5/23/2024 07:43:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.