Loading...

Bashe, Jafo wapewa jukumu maalum uzalishaji sukari

Rais Samia Suluhu Hassan (Picha: Ikulu)

Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Selemani Jafo kuanza mchakato wa mabadiliko ya sera ili viwanda vya sukari vya ndani viwe na uwezo wa kuzalisha sukari ya viwandani na malighafi ya kuzalisha nishati safi ya kupikia na matumizi mengine.

Vilevile, Rais ameagiza Chuo Kikuu cha Mzumbe kurejesha utaratibu wa kufundisha viongozi wa serikali ili kuongeza uwajibikaji na kupata watumishi wanaotekeleza majukumu yao kwa weledi na ufanisi mkubwa.

Rais Samia aliagiza hayo jana kwa nyakati tofauti wakati akizungumza na wananchi katika ziara yake mkoani Morogoro baada ya kufungua mradi wa ujenzi wa barabara ya Kidatu-Ifakara yenye urefu wa kilometa 66.9 na daraja la Mto Ruaha Mkuu, kuweka jiwe la msingi wa ujenzi wa jengo la Chuo Kikuu cha Mzumbe na kufungua mradi wa upanuzi wa Kiwanda cha Sukari Kilombero.

Alisema kama viwanda vya sukari vya ndani vikizalisha sukari ya viwandani, vitaipunguzia serikali matumizi ya fedha za kigeni kuagiza bidhaa hiyo nje ya nchi na hivyo kusaidia kukabili uhaba wa dola nchini.

Alisema mahitaji ya sukari ya nyumbani ni tani 650,000 huku ya viwandani ikiwa ni tani 250,000 na kwamba kuendelea kuagiza bidhaa hiyo nje ya nchi ni matumizi mabaya ya fedha za kigeni.

"Nina uhakika tukivipa kazi viwanda vyetu vinaweza kutuzalishia sukari ya viwandani na hiyo sasa ndio kazi ninayotaka mkaifanyie kazi, angalieni mtawekaje sera zetu ili viwanda hivi vizalishe sukari ya viwandani, lakini pia wazalishe ‘Ethanol’ kwa ajili ya kupata nishati safi ya kupikia na viwanda vingine," aliagiza.

Rais alimwagiza Waziri wa Kilimo (Bashe) kujadiliana na wazalishaji sukari changamoto zilizopo kwa upana na kuzitatua ili kuwawekea mazingira mazuri ya uzalishaji, lengo likiwa ni kuhakikisha nchi inajitosheleza kwa chakula.

Rais Samia alisema serikali ipo tayari kubadilisha sera na sheria za nchi ili kuweka mazingira mazuri ya wawekezaji, lengo likiwa kujihakikishia uzalishwaji chakula cha kutosha kwa mahitaji ya ndani na nje.

Akiwa katika Jimbo la Mikumi, Rais alishauri wananchi wa eneo hilo kuwekeza katika nyumba za wageni ili kujiongezea kipato kutokana na ongezeko la watalii linalosababishwa na matangazo aliyoyafanya kupitia filamu ya Tanzania The Royal Tour pamoja na treni ya kisasa ya mwendokasi.

Rais pia alisema serikali imetenga Sh. bilioni 7.2 kwa ajili ya kuendeleza Bonde Ruhembe, fedha hizo zitatumika kufanya utafiti, kujenga mabwawa kwa ajili shughuli za kilimo ikiwamo mpunga na miwa na kujenga kingo zitakazodhibiti mafuriko.

Alisema itendelea kuwapa wakulima ruzuku ya mbolea na inajipanga kwa ajili ya kuwapa ruzuku za mbegu, ili kupunguza changamoto zitokanazo na uzalishaji mazao ili nao wafurahie matunda ya kazi zao.

Alipongeza Watanzania kwa kazi nzuri ya kuongeza uzalishaji chakula kwa kuwa kwa mara ya kwanza mwaka huu nchi imeuza tani milioni 1.1 za chakula Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na tani 600,000 zimeuzwa Zambia.

Akiwa Mzumbe, Rais aliagiza chuo kikuu hicho kurejesha utaratibu wa kufundisha viongozi wa serikali ili kuzalisha viongozi zaidi wanaofanya kazi kwa weledi na ufanisi huku akiahidi kukitafutia fedha zaidi chuo hicho.

"Mzumbe ni Chuo chenye sifa ya kupika na kuzalisha viongozi mbalimbali wakiwamo wa Chama chetu cha Mapinduzi (CCM), kwa haraka Dk. Emmanuel Nchimbi na kwa upande wa serikali ni Balozi Ombeni Sifue ambaye bado tunamtumia kwenye shughuli za kiserikali," alisema.

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, alisema mahitaji ya sukari kwa sasa ni tani laki 650,000, upanuzi wa kiwanda hicho utaongeza uzalishaji hadi kufikia tani 271,000 kwa mwaka na idadi ya wakulima kutoka 9,500 mpaka 16,000 na mapato ya wakulima yatapanda kutoka Sh. bilioni 65 hadi bilioni 165.

Alisema wameanza kufanya upembuzi yakinifu wa kuwawekea wakulima wa miwa miundombinu ya umwagiliaji ili wafikie tija ya uzalishaji wa angalau tani 80 hadi 100, lengo likiwa ni asilimia 65 wa miwa ya kutumika katika uzalishaji sukari itoke kwa wazalishaji wadogo.

Msajili wa Hazina, Nehemia Msechu, alisema serikali inamiliki uwekezaji wa kiwanda hicho kwa asilimia 25 kupitia ofisi yake.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. Willium Mwegoha, alisema ujenzi wa majengo mapya chuoni umeshaanza na utagharimu Sh. bilioni 4.8 na kuongeza udahili wa wanafunzi kutoka 15,000 hadi kufikia 40,000.
Bashe, Jafo wapewa jukumu maalum uzalishaji sukari Bashe, Jafo wapewa jukumu maalum uzalishaji sukari Reviewed by Zero Degree on 8/05/2024 09:38:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.