Loading...

Dabo: Licha ya uwanja mzima kuisapoti Rayon, lakini wachezaji wangu hawakujali


Bao la dakika ya 57 lililofungwa na beki Lusajo Mwaikenda, liliipa timu ya Azam FC ushindi wa 1-0 dhidi ya Rayon Sport katika mechi maalum ya kimataifa ya kirafiki iliyochezwa juzi katika Uwanja wa Pele, Kigali nchini Rwanda.

Timu zote mbili ziliitumia mechi hiyo kutambulisha wachezaji wake wa msimu mpya, ambapo Azam iliita tamasha hilo Azamka, na wenyeji walilipa jina la Rayon Sport Day, ambapo kabla ya mechi kulikuwa na burudani kadhaa.

Kocha Robert Oliveira maarufu kwa jina la Robertinho, alionekana kwa mara ya kwanza akiifundisha timu hiyo, baada ya kuondoka Simba mwanzoni mwa Januari mwaka jana.

Pia katika mechi hiyo, ilishuhudiwa kiungo mshambuliaji wa Yanga, Haruna Niyonzima, akiichezea timu ya Rayon.

Kocha wa Azam FC, Youssouph Dabo, amesema ilikuwa ni mechi nzuri ambayo imewapa kipimo tosha kuelekea kwenye mchezo wa awali wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya APR utakaochezwa Agosti 23 hadi 25, mwaka huu nchini humo.

"Ilikuwa mechi nzuri na kuna wakati ilikuwa ngumu sana kwetu, lakini ilikuwa ni jambo jema kupata mchezo kama huu kwa sababu ilikuwa ni muhimu kuja hapa kusoma mazingira ambayo yatatusaidia kwenye mechi yetu inayokuja dhidi ya APR, Ligi ya Mabingwa Afrika, na kiwango kilikuwa kizuri tu.


"Umeona uwanja mzima ulikuwa unaisapoti Rayon Sport, hata hivyo wachezaji wangu hawakujali na hii imetupa kujiamini katika mchezo wetu unaokuja," alisema Dabo.

Kwa upande wa Robertinho, alisema ndiyo kwanza ana siku tano tangu aitwae timu hiyo, akiahidi kufanya marekebisho ingawa kikosi chake kilicheza vema.

"Nimeanza kazi siku tano tu zilizopita, lakini wachezaji wangu wamepambana nawapongeza, kipindi cha kwanza tumecheza vema, kipindi cha pili pia, lakini tukajisahau ndani ya boksi tukafungwa bao," alisema raia huyo wa Brazil.
Dabo: Licha ya uwanja mzima kuisapoti Rayon, lakini wachezaji wangu hawakujali Dabo: Licha ya uwanja mzima kuisapoti Rayon, lakini wachezaji wangu hawakujali Reviewed by Zero Degree on 8/05/2024 12:13:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.