Sekta binafsi mshirika mkubwa wa Serikali katika kutekeleza agenda ya Nishati Safi ya Kupikia
Imeelezwa kuwa, Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (EU) na Washirika wengine wa Maendeleo wamekuwa msaada mkubwa katika kusaidia Ajenda ya Nishati Safi ya kupikia kuzidi kusonga mbele hapa nchini.
📌 Upatikanaji Nishati Safi ya Kupikia kufika hadi ngazi ya Kaya
📌Asisitiza kuisukuma ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia
📌Asilimia 80 ya Watanzania kutumia Nishati Safi ifikapo 2034
📌Serikali kuendelea kushirikiana na UNCDF NA EU
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga wakati akimwakilisha Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko katika Warsha ya Nishati Safi ya Kupikia iliyoanza Juni 19, 2024 jijini Dar es Salaam.
"Serikali inatambua michango ya programu mbalimbali zinazotekelezwa na washirika wa maendeleo na sekta binafsi ikiwemo ya mradi wa CookFund unaoendelea katika nchi yetu. Katika kuendeleza sekta hii, tuko tayari kuendelea kushirikiana na UNCDF na wadau wengine wa nishati safi ya kupikia." Amesema Mhe. Kapinga.
Aidha, amewataka wadau kushirikiana na serikali ili kwa pamoja kutafuta na kupendekeza mikakati ambayo itaharakisha lengo la nchi la asilimia 80 ya watanzania kutumia Nishati Safi ya Kupikia ifikapo 2034.
Amesisitiza kuwa, kila mmoja ana jukumu muhimu katika kufanikisha maendeleo ya soko na teknolojia zinazohitajika kufikia lengo hilo la asilimia 80 ya Watanzania kuhamia kwenye Nishati Safi ifikapo 2034 kama ilivyoainishwa kwenye Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia.
"Warsha hii ni moja ya utekelezaji wa maagizo ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa uzinduzi wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi 2024 - 2034, ambapo aliagiza Wizara ya Nishati kukaa pamoja na wadau wa Nishati Safi ya Kupikia na kuzungumzia kuhusu itakavyoweza kufikia kwa pamoja malengo ya mkakati wa nishati safi ya kupikia" Amesisitiza Mhe. Kapinga.
Vile vile, amewataka wadau katika kuelekea katika matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kuwa wabunifu, waoneshe juhudi na kudumusha ushirikiano miongoni mwa wadau wa sekta ili kufikia lengo.
Ameongeza kuwa, Serikali itaweka mazingira wezeshi ya upatikanaji wa Nishati Safi ya Kupikia kwa kila kaya ili kuimarisha afya ya umma na maendeleo endelevu katika Sekta ya mazingira na uchumi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shirika la UNCDF nchini, Peter Malika amesema wanashirikiana na Serikali katika nyanja mbalimbali ikiwemo mfuko wa CookFund unaolenga kuimarisha Nishati Safi ya Kupikia. Amesema Nishati Safi ni fursa na biashara ambapo aliwataka wadau mbalimbali kuichangamkia fursa hiyo kwa sasa.
Mkutano huo umewakutanisha wadau mbalimbali, wakiwemo Watunga Sera, Wadau wa Maendeleo, Wabunifu, Sekta Binafsi na Washirika wa Kimataifa.
Sekta binafsi mshirika mkubwa wa Serikali katika kutekeleza agenda ya Nishati Safi ya Kupikia
Reviewed by Zero Degree
on
6/19/2024 04:05:00 PM
Rating: