Loading...

Zaidi ya wanachama 200 ACT wamejiunga na CCM

Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi akionesha kadi za wananchama wa ACT Wazalendo ambao wamehamia CCM

Wanachama zaidi ya 200 wa Chama cha ACT- Wazalendo wakiongozwa na Mwenyekiti wao Mkoa wa Lindi, Hamidu Bobali, wamejiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Wanachama hao walipokewa jana na Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, wakati akihutubia wanachama wa CCM na wananchi katika Uwanja wa Mpilipiki, mkoani Lindi.

Akizungumza katika mkutano huo kwa niaba ya wanachama hao, Bobali alisema sababu iliyowasukuma kuhamia CCM ni kazi nzuri iliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan katika uongozi wake, mkoani Lindi.

Alisema tangu alipohamia ACT- Wazalendo akitoka Chama cha Wananchi (CUF) amekuwa haoni maendeleo yoyote ndani ya chama hicho.

"Kwa miaka mitatu Rais Samia ameibadilisha Lindi, ameleta maendeleo katika sekta ya maji, kilimo, elimu pamoja na miundombinu. Sasa leo mimi na kundi langu tumeamua kumfuata (Samia), ili kumsaidia kuisukuma Lindi iwe na maendeleo," alisema Bobali.

Akizungumza katika mkutano huo baada ya kuwapokea wanachama hao, Balozi Dk. Nchimbi alisema kwa miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia, Lindi imefanikiwa kujenga hospitali nne, vituo vya afya 18 pamoja na zahanati 41.

Alisema katika sekta ya elimu serikali katika miaka mitatu imefanikiwa kujenga shule 54 za serikali na binafsi pamoja na kufanikisha kuandikisha idadi kubwa ya wanafunzi pamoja na kuongeza ufaulu.

Dk. Nchimbi alisema serikali itaendelea kutatua matatizo yanayowasibu wakazi wa Lindi, ikiwamo kulipa fidia kwa wakati wananchi wanaoathiriwa na wanyama hususani tembo.

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla, aliwataka wananchi wa Lindi kutofanya makosa ya kuchagua viongozi wa upinzani kama walivyofanya katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2010 na 2015.

Alisema Jimbo la Lindi limekuwa likileta shida wakati wa uchaguzi kwa vyama vya upinzani kushinda kuanzia ngazi ya kata hadi jimbo.

Makalla alisema: "Katika uchaguzi wa mwaka 2010 kuna mtu aliongoza hapa Lindi anaitwa Baruani. Nikadhani CCM tumejisahau kidogo, lakini tulipofanya uchaguzi wa mwaka 2015 hali ikawa mbaya zaidi katika majimbo manane tulipoteza majimbo manne. Majimbo tuliyopoteza ni Kilwa yote Kusini na Kaskazini, tukapoteza Liwale pamoja na Mchinga."

Makalla alisema chama kilichokuwa kinashinda katika Jimbo la Lindi ni Chama cha Wananchi CUF, aliwataka wananchi wa Lindi kutorudia makosa waliyokuwa wanayafanya katika chaguzi zilizopita.

Kadhalika, aliwaagiza viongozi wa CCM mkoani Lindi kuhakikisha katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vitongoji na Kata, CCM inaibuka mshindi kwa kishindo.

Mbunge wa Lindi Mjini, Hamida Abdallah alimwomba Dk. Nchimbi kusaidia ujenzi wa Shule ya Sekondari Lindi iliyoungua moto miaka mitano iliyopita.

Alisema ameshawasiliana na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), lakini bado hajapata majibu ya uhakika hivyo kupitia kwa Dk. Nchimbi anaamini jambo hilo linakwenda kutekelezwa kwa uharaka.

Katibu wa NEC, Idara ya Mambo ya Ndani ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa (SUKI), Rabia Abdallah Hamid, alisema Rais Samia amefanya mambo makubwa katika uongozi wake wa miaka mitatu.

Alisema Samia amefanikisha kupanda bei ya zao la ufuta pamoja na mbaazi, kwamba zao la korosho serikali imeshaweka mikakati kuhakikisha nalo linakuwa na bei nzuri kwa wakulima.
Zaidi ya wanachama 200 ACT wamejiunga na CCM Zaidi ya wanachama 200 ACT wamejiunga na CCM Reviewed by Zero Degree on 7/31/2024 10:14:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.