Loading...

Historia yaandikwa utekelezaji Mradi wa Chuma Maganga Matitu

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema mafanikio hayo yametokana na jitihada za Serikali kuchochea matumizi sahihi ya rasilimali kwa manufaa ya Watanzania

📌 Ni Mradi wa Dola Milioni 77 kwa Maendeleo ya Viwanda Nchini

📌 Utafiti Waonesha Uwepo wa Tani Milioni 101 za Chuma

📌 Dkt. Biteko Ahimiza Wananjombe Kutumia Fursa za Mradi

📌TANESCO, REA Wapewa Siku 5 Kushauri Namna ya Kufikisha Umeme Vijiji 10 Ludewa

Tanzania imeandika historia mpya ya matumizi ya rasilimali zake kufuatia kusainiwa kwa utekelezaji wa mradi wa uchimbaji wa chuma wenye thamani ya dola milioni 77.

Mradi huo ambao utatekelezwa katika eneo la Maganga Matitu Wilayani Njombe unatarajiwa kuchochea maendeleo ya viwanda nchini na hivyo kukuza uchumi wa nchi.

Akizungumza Agosti 2, 2024 mkoani Njombe mara baada ya kushuhudia utiaji saini wa Mkataba wa Uchimbaji Madini ya Chuma Maganga Matitu kati ya Shirika la Maendeleo la Taifa NDC na Kampuni ya Fujian Hexingwang Industry Tanzania .Co.Ltd. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema mafanikio hayo yametokana na jitihada za Serikali kuchochea matumizi sahihi ya rasilimali kwa manufaa ya Watanzania.

‘‘Mhe. Rais amekuwa muumini wa kuikaribisha sekta binafsi iweze kushiriki kwenye uchumi wa nchi yetu ili tupate kodi na ajira kwa vijana wetu. Mradi huu na mingine mtaona dhamira yake ya kuona chuma kinachimbwa na kinapatikana,” anasema Dkt. Biteko.

Anasisitiza ‘‘Ndio maana haikushangaza kulipa fidia bilioni 15 ili kupisha mradi wa Liganga na Mchuchuma ambao ndio mradi mkubwa katika bara la Afrika tunaoutegemea. Nataka niwahakikishie watu wa Ludewa na Njombe mambo mengi zaidi yanakuja tuendelee kumuombea Rais Samia.”

Pia ameipongeza Wizara ya Viwanda na Biashara kwa usimamizi katika hatua iliyofikiwa.

Aidha, Dkt. Biteko amesema kuwa Serikali imekuwa ikijenga madaraja na miradi mingine mikubwa kwa kutumia chuma kutoka nje ya nchi ilihali kuna utajiri mkubwa wa chuma kwenye ardhi ya Tanzania.

Ametoa wito kwenye miradi mingine yote inayotekelezwa nchini na kusema kuwa Watanzania wanataka kuona rasilimali zilizopo kwenye maeneo yao zinaleta maana kwenye maisha yao na kuwa utaratibu wa kuwa na rasilimali eneo fulani au kuchimbwa lakini sherehe za utiaji asaini mikataba au uzinduzi zinafanyika Dar es salaam au Dodoma kuwa si sawa ni lazima kwenda kwa wananchi wenyewe na kufanya jambo hilo kwa.

‘‘Niwaombe wawekezaji muwe na hakika kuwa hakuna hasara mtakayopata katika kuwekeza Tanzania kwa sababu nchi yetu ina mazingira mazuri ya kibiashara na mahali tunapodhani kuna changamoto Mhe. Rais amekuwa akiunda kamati ili kurekebisha kasoro ndani ya mifumo ya Serikali, mtakumbuka kuna wakati haki jinai ilikuwa inalamikiwa na aliunda kamati na mapendekezo yake yanafanyiwa kazi na sasa ameunda tume ya kupitia malalamiko ya kodi, ’’amebainisha Dkt. Biteko.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amelitaka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Umeme Vijijini (REA) kufanya utafiti na kuwasilisha mapendekezo ya namna ya kufikisha umeme katika vijiji 10 vilivyopo pembezoni mwa Ziwa Nyasa eneo lenye milima wilayani Ludewa.

‘Nimekuja na wataalamu kutoka TANESCO na REA na nitaomba Mkuu wa Mkoa tupate mwakilishi kutoka Ludewa nataka tuunde timu ili tukapitie upya vijiji kisha tujadiliane na kukubaliana namna ya kufikisha umeme katika vijiji hivyo kama ni kwa kujenga njia kubwa ya umeme au kuweka gridi. Kazi ianze Jumatatu na ndani ya siku tano nipate majibu tujenge kwa namna gani.’’ Amesema Dkt. Biteko.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exhaud Kigahe amesema kuwa mwaka 2023, Rais Mhe. Dkt. Samia alilipa fidia ya takribani shilingi bilioni 15 kwa wananchi waliopisha maeneo yao kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo na mwaka 2020 aliahidi kutekelezwa kwa shughuli za uchumi ili maeneo yote ya uwekezaji yaweze kufanikiwa na sasa anamitiza ahadi yake.

‘‘Uhakiki wa taarifa za mashapo uliofanyika mwaka 2020 katika mradi huu wa Maganga Matitu umeonesha uwepo wa mashapo ya chuma tani milioni 101 na utekelezaji wa mradi huu utaongeza mnyororo wa thamani utakaokuza uchumi wa viwanda sasa utawezesha Serikali kuokoa fedha za kigeni zilizokuwa zikitumika kwa ajili ya kuagiza chuma kutoka nje ya nchi.’’ Amesema Mhe. Kigahe.

Naye, Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo (NDC), Dkt. Nicolous Shombe amesema kuwa mradi huo wa kuzalisha chuma wa Maganga Matitu ni mradi mdogo ukilinganisha ule wa Mchuchuma na Liganga ambao tangu kuamuliwa kutekelezwa mwaka 2007 hadi kufikia hatua ya sasa ni takribani miaka 17.

‘‘Sasa tunaenda kutekeleza mradi huu ambao Serikali itakuwa na asilimia 36 mwekezaji kutoka nchini China atakuwa na asilimia 64, kwa kiasi kikubwa katika mradi huu Serikali inaenda kuhusika moja kwa moja kulingana na muundo wake wa menejimenti na bodi,’’amesema Dkt. Shombe.

Ameongeza ‘‘ Mradi huu utazalisha chuma ghafi ambacho kitatumiwa na vyuma vingine na hivyo tutakuwa na uchumi shindani kwa kuzalisha vyuma vitakavyotumika katika miradi mikubwa ya miundombinu. Katika mradi huu tunatarajia kuwekeza zaidi ya dola milioni 77.45 ambazo ni fedha za mtaji kutoka kwa mwekezaji na uzalishaji utaanza mwaka 2027, wananchi 385 watalipwa fidia kabla ya mwezi Januari ambayo ni zaidi ya shilingi bilioni 4.25.’’

Vilevile, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Fujian Hexingwang Industry Tanzania .Co.Ltd. Bw. Ix Xsinda amesema kuwa Kampuni yake imewekeza nchini kwa miaka nane na kuwa inamiliki kiwanda cha nondo kilichopo Mkuranga mkoani Pwani.

‘‘Namshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali kwa ujumla kwa kuniamini ili niweze kufanya uwekezaji huu, kwa upekee nawashukuru NDC kwa kuhakikisha nafanikiwa kuwekeza katika mradi nawahakikishia wananchi wa Njombe kwamba nitawekeza katika mradi huu kama tulivyokubaliana katika mkataba kwa sababu Mhe. Rais na Serikali yake wamenipa imani kubwa. Nitaanza utekelezaji baada ya kusaini mkataba huu na taratibu zingine kukamilika.’’ Amemaliza Bw Xsinda.

Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka amesema kuwa Mkoa wake utahakikisha unaweka mazingira rafiki kwa wawekezaji watakaowekeza mkoani humo.








(Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati)
Historia yaandikwa utekelezaji Mradi wa Chuma Maganga Matitu Historia yaandikwa utekelezaji Mradi wa Chuma Maganga Matitu Reviewed by Zero Degree on 8/03/2024 08:01:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.