Loading...

Dkt. Biteko atoa wito Vyombo vya Habari kuelimisha jamii kuhusu mashujaa


📌Rais Samia mgeni rasmi Maadhimisho ya Mashujaa kesho

📌Atoa wito kwa wananchi kushiriki Maadhimisho ya Mashujaa

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ametoa wito kwa vyombo vya habari kushirikiana na Serikali katika kuelimisha jamii kuhusu historia ya mashujaa nchini.

Dkt. Biteko ametoa wito huo Julai 24, 2025 katika Uwanja na Mnara wa Mashujaa uliopo Mji wa Serikali, Mtumba jijini Dodoma mara baada ya kukagua maadalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Mashujaa.

“Ninatoa wito kwa wananchi wote kushiriki kwa wingi kwenye tukio hili adhimu. Hii ni siku yetu sote, siku ya kumkumbuka Mtanzania mwenzetu aliyesimama kwa ajili ya Taifa. Vivyo hivyo, nawaomba nyinyi waandishi wa habari, pamoja na vyombo vyenu na pia mitandao ya kijamii mshirikiane na Serikali katika kuelimisha jamii kuhusu historia ya mashujaa wetu, thamani ya mchango wao, na sababu ya sisi kuendelea kuwakumbuka kila mwaka,” amesema Dkt. Biteko.

Amezungumzia maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Mashujaa na kusema kuwa yanaendelea vizuri na mgeni rasmi katika tukio hilo anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, huku akisisitiza kuwa siku hiyo ni maalum kwa ajili ya kuwakumbuka, kuwaenzi na kuwaheshimu mashujaa wetu waliotoa maisha yao, nguvu zao, na sadaka zao kwa ajili ya uhuru, amani na maendeleo ya Taifa.

Amefafanua kuwa kwa heshima hiyo, saa 6:00 usiku wa tarehe 24 Julai, 2025 siku moja kabla ya kilele cha maadhimisho, Mwenge wa Kumbukumbu ya Mashujaa utawashwa rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule kwa niaba ya Rais kuashiria kuanza kwa maombolezo ya Mashujaa wetu.

Ameongeza kuwa katika siku ya maadhimisho kesho tarehe 25 Julai, 2025 kuanzia saa 3:00 asubuhi kutakuwa na gwaride rasmi la heshima litakalofanywa na Vikosi vya Ulinzi na Usalama. Aidha, saa 6:00 usiku wa tarehe hiyohiyo mwenge wa Kumbukumbu ya Mashujaa utazimwa rasmi kuashiria hitimisho la maombolezo ya kumbukumbu Mashujaa kwa mwaka 2025.

Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa hufanyika kila mwaka tarehe 25 Julai 2025 kwa lengo la kuwakumbuka mashujaa waliopoteza maisha yao katika uwanja wa vita, waliostaafu baada ya kulitumikia Taifa kwa uaminifu, na wale waliopata majeraha katika kuilinda nchi yetu.







Dkt. Biteko atoa wito Vyombo vya Habari kuelimisha jamii kuhusu mashujaa Dkt. Biteko atoa wito Vyombo vya Habari kuelimisha jamii kuhusu mashujaa Reviewed by Zero Degree on 7/24/2025 01:10:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.