Loading...

JPM atoa siku 5 kwa TANROAD



Rais Dkt. John Magufuli ametoa siku tano kwa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kuhama katika jengo walilopanga na kuhamia katika jengo la Serikali.

Magufuli ametoa uamuzi huo leo Jumapili, Oktoba 6, 2019 na kumweleza Mtendaji Mkuu wa tanroad Patrick Aron Nipilima Mfugale wakati akizungumza na wananchi wa Sumbawanga wakati wa kuzindua Barabara ya Tunduma – Sumbawanga yenye urefu wa kilomita 223.1 katika eneo la Laela mkoani Rukwa.

Aidha, Magufuli ametoa mwezi mmoja kwa Watendaji akiwamo Mkurugenzi na Meya wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa kuhamisha makazi yao kutoka Sumbawanga Mjini na kuhamia katika mji mdogo wa Laela ili iwe rahisi kuwahudumia wananchi wa maeneo hayo.

Pia, ametoa mwezi mmoja kwa taasisi nyingine za Serikali zilizopanga kwenye majengo ya watu binafsi kuhamia majengo ya serikali.

“Kuna taasisi zimepanga kwenye nyumba mojawapo ni Tanroads, mnalipa Sh2 bilioni, nawapa ndani ya siku tano muhamie majengo ya Serikali. Najua kuna watu wamepanga kwa ajili ya asilimia zao sasa hatuwezi kuendesha nchi kwa mtindo huu, nimetoa muda huo muhame.

“Na sio TANROADS tu bali Taasisi zingine zote Tanzania ambazo zimepanga kwenye nyumba binafsi kwaajili ya asilimia fulani wahame mara moja wakakae katika Nyumba za serikali.

“Kuna Halmashauri ya Sumbawanga na ya Manispaa, ofisi zote huzi zipo Sumbawanga Mjini. Nataka Halmashauri ya Sumbawanga Vijijini mhame hiyo ofisi huko mjini, anayetaka ukurugenzi ahame huko aje apange hapa, hatuwezi kwenda kwa michezo ya kipumbavu namna hii,” amesema Magufuli.

Ofisi za Tanroads zipo katika Jengo la Airtel Moroco jijini Dar es Salaam.
JPM atoa siku 5 kwa TANROAD JPM atoa siku 5 kwa TANROAD Reviewed by Zero Degree on 10/06/2019 03:20:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.