Loading...

Miraji atoa siri ya tuzo Simba SC


MSHAMBULIAJI wa Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba, Miraji Athumani, amesema amerudi katika klabu hiyo ili aweze kutimiza ndoto zake za kufika mbali katika mchezo huo unaopendwa na watu wengi duniani.

Miraji maarufu kama 'Shevchenko', wengi wakimuita kwa kifupi "Sheva", kama wenzake wanavyomuita tangu akiwa Simba B, amesema hayo baada ya kuchaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mwezi Septemba mwaka huu.

Mshambuliaji huyo aliyerejea Simba akitokea Lipuli FC, amefunga mabao mawili kati ya 10 ambayo yamefungwa na mabingwa hao watetezi kwenye mechi nne walizocheza msimu huu.

Kwa mujibu wa taarifa ya Nipashe, Miraji, alisema kuwa kila atakapopata nafasi ya kucheza, atakuwa anajituma kwa sababu mawakala na makocha mbalimbali wa kigeni wanaiangalia zaidi Simba kuliko timu nyingine inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.

Miraji alisema pia anashukuru ushirikiano na umoja anaoupata katika kikosi cha Simba na anaamini hali hiyo ikiendelea, ataifanyia makubwa zaidi.

"Namshukuru Mungu nimepata tuzo ya kwanza ya Ligi Kuu, ni tuzo ambayo kila mchezaji amekuwa na ndoto nayo, lakini ushirikiano kutoka kwa wachezaji wenzangu ndio umenifikisha hapa nilipo ,naamini nitafanya mengi zaidi katika mechi zinazokuja," alisema Miraji.

Mbali na Miraji, Kocha Mkuu wa Simba Mbelgiji Patrick Aussems naye alichaguliwa kuwa Kocha Bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara Septemba, kwa kutwaa tuzo hizo, kila mmoja atapata zawadi ya Sh. milioni moja kutoka kwa wadhamini wa tuzo hiyo.
Miraji atoa siri ya tuzo Simba SC Miraji atoa siri ya tuzo Simba SC Reviewed by Zero Degree on 10/07/2019 07:35:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.