Maandamano Haiti kuhusu wizi wa kura za urais
Hali katika mji mkuu wa Haiti ni tete baada ya wafuasi wa mgombea mmoja wa kiti cha urais kuzusha rabsha.
Waandamanaji hao wafuasi wa mgombea maarufu wa kiti cha urais nchini Haiti wamewasha moto magurudumu ya magari na kuweka vizuzi mabarabarani.
Wanaiishtumu tume ya uchaguzi nchini humo kwa kukiuka kanuni na utendaji wa uchaguzi huru na wa haki.
Waandamanaji hao walijitokeza mabarabarani baada ya mgombea wanaomuunga mkono Moise Jean-Charles, kudai kuwa kura zake zimeteketezwa moto ama kufichwa.
Seneta huyo wa zamani ameishtumu tume ya uchaguzi kwa kupendelea mgombea mmoja na hivyo kupanga njama ya kupunguza idadi ya kura zake.
Hayo yametokea licha ya uchaguzi mkuu wa urais kulindwa kwa kiasi kikubwa mno na walinda usalama wa umoja wa mataifa.
Waangalizi wa umoja wa matafa wamesifu utendaji kazi wa tume hiyo ya uchaguzi wakisema kuwa kwa kiasi kikubwa uchaguzi huo ulikuwa wa haki .
Hata hivyo maafisa wamepigwa na butwaa baada ya madai hayo ya kuibiwa kura kuibuka na sasa wameanzisha uchunguzi kutathmini ukweli wake.
Matokeo ya kimsingi yanatarajiwa kutangazwa juma lijalo.
Madai ya watu kuruhusiwa kupiga kura zaidi ya mara moja yameibuka huku wengine wakidai kuwa kulikuwa na njama ya kutoa vitambulisho ghushi za kupigia kura.
Afisa mmoja wa Polisi alifumaniwa akiendesha gari lililokuwa limejaa makaratasi ghushi ya kura ambayo yalikuwa yameshajazwa.
Credits: BBC
Maandamano Haiti kuhusu wizi wa kura za urais
Reviewed by Zero Degree
on
10/30/2015 11:04:00 AM
Rating: