Loading...

Baraza dogo la Rais John Magufuli

Dar es Salaam. Ahadi ya Rais John Magufuli kuwa ataunda Baraza dogo la Mawaziri imejenga shauku ya Watanzania kufahamu kiwango cha ukubwa au udogo wa baraza hilo ikilinganishwa na mabaraza yaliyoundwa na watangulizi wake baada ya kuapishwa, tangu Tanzania ipate Uhuru mwaka 1961.
Baraza hilo la Dk Magufuli ambalo Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema litatangazwa muda ukifika, tayari limechukua muda mrefu zaidi kuandaliwa, ikilinganishwa na mabaraza ya kwanza ya marais waliomtangulia tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini.

Changamoto inayomkabili Rais Magufuli ni kuunda baraza litakalokidhi matarajio yake na kauli mbiu yake ya “Hapa ni Kazi Tu” na matarajio ya Watanzania kwa upande mmoja na ahadi yake kwa upande mwingine, ya kuwa na baraza dogo.

Akilihutubia Bunge mjini Dodoma hivi karibuni na wakati akiwa katika mikutano yake ya kampeni za Uchaguzi Mkuu, Dk Magufuli aliahidi kuunda baraza dogo ikiwa ni njia za kudhibiti matumizi ya Serikali kwa nia ya kutafuta majawabu ya kero za wananchi kwa kasi inayostahili.

Kutokana na ahadi yake, jambo ambalo halitarajiwi ni Dk Magufuli kuteua mawaziri, idadi sawa na alioanza nao mtangulizi wake, Rais Jakaya Kikwete aliyevunja rekodi ya kuunda Baraza kubwa kuliko marais wote waliomtangulia tangu Uhuru.

Baraza hilo alilounda Kikwete mwaka 2005 baada ya kuingia madarakani, lilikuwa na mawaziri 60, kati yao 29 walikuwa mawaziri kamili na 31 naibu mawaziri.

Kinyume chake, Serikali ya Awamu ya Kwanza ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ndiyo iliyovunja rekodi ya kuwa na Baraza dogo la mawaziri 11 mwaka 1961.

Katika awamu ya pili mwaka 1985, Rais Ali Hassan Mwinyi alipoingia madarakani aliunda Baraza la Mawaziri lenye mawaziri 23 na manaibu wanane, jumla walikuwa 31.

Mwaka 1995, Rais Benjamin Mkapa alianza na mawaziri 27 na naibu mawaziri 10, jumla walikuwa 37 na aliowaita askari wa miamvuli.

Soma Kauli ya wasomi

Wachambuzi wa masuala ya siasa na utawala wanapendekeza kuwa kutokana na mahitaji ya sasa na jitihada za kubana matumizi, Baraza lingefaa kutozidi mawaziri 20.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana alisema ukubwa au udogo wa baraza unategemea na vipaumbele vya Rais katika kipindi chake cha uongozi kama vitakidhi mahitaji ya Watanzania.

“Haiwezekani kuwa na wizara 10 au chini ya hapo kutokana na ukubwa wa nchi na utendaji kazi wa Serikali kwa sasa, lakini sidhani kama kuna haja ya kuzidisha zaidi ya wizara 20,” alisema.

Kauli hiyo imeshabihiana na aliyoitoa Mhadhiri wa Chuo kikuu cha Mzumbe, Profesa George Shumbusho kuwa kulingana na mahitaji ya wananchi kwa sasa, hakuna haja ya kuwa na wizara zaidi ya 22.

Alisema udogo wa baraza hilo utategemea na namna ambavyo Rais Magufuli atapunguza na kuunganisha wizara zisizokuwa na uzito.

“Kuna wizara ambazo hata zikipunguzwa hazina athari na zinaweza kuvunjwa au kuunganishwa kwa ufanisi zaidi,” alisema. Mapendekezo ya wachambuzi hao yanaenda sanjari na yale yaliyokuwa katika Rasimu ya Katiba Mpya ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo ibara ya 93(2) ilikuwa imependekeza Baraza la Mawaziri lisizidishe watu 15.

Hata hivyo, pendekezo hilo lilitupiliwa mbali wakati wa kujadili rasimu hiyo katika Bunge la Katiba ambalo lilifanikisha kuanzishwa kwa Katiba Inayopendekezwa inayosubiri kupigiwa kura ya maoni.


Credits: Mwananchi




Mshirikishe na mwnzako kuhusiana na habari hii!!!
Baraza dogo la Rais John Magufuli Baraza dogo la Rais John Magufuli Reviewed by Zero Degree on 12/06/2015 01:52:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.