Loading...

BOMOA BOMOA: Nyumba zaidi ya 5000 kuvunjwa Dar!!!

Dar es Salaam. Vilio, simanzi, majonzi na nyuso zilizojaa huzuni vilitawala Bonde la Mto Msimbazi wilayani Kinondoni jana wakati nyumba zilizojengwa kinyume cha sheria zilipokuwa zikibomolewa.

Bomoabomoa hiyo iliyoanza kutikisa juzi, imezifikia zaidi ya nyumba 200 kati ya 5,600 zinazotarajiwa kubomolewa jijini Dar es Salaam.

Watakaokumbwa na shughuli hiyo ni wananchi wote waliovamia na kujenga nyumba zao kwenye mabonde, maeneo ya wazi, hifadhi za mito na fukwe za Bahari ya Hindi.

Mwananchi ilishuhudia baadhi ya wanawake na watoto wakiangua vilio mithili ya msiba bila kujua ni wapi watakwenda, licha eneo hilo kukumbwa na mafuriko kila mvua zinaponyesha.

“Sijui wapi nitaelekea na watoto hawa wadogo, mume wangu alinitelekeza na hapa nilipo sina hata pesa kwenye akiba yangu. Mungu kwanini mimi? Uliniumba nifanye nini hapa duniani? Ona ninateseka na viumbe wako hawa,” alisema Huzra Hassan, huku akibubujikwa na machozi.

Huku akisaidiwa na majirani, ambao pia walikumbwa na mkasa huo, Huzra aliiomba Serikali kumsaidia eneo jingine atakalojenga ili aishi na wanae.


Hali ilikuwa mbaya zaidi kwa familia ya Mzee Athman Salehe, anayeuguliwa na mkewe kwenye nyumba iliyo eneo hilo.

“Nyumba yangu huwa inajaa maji kila inaponyesha mvua, hali yetu ya maisha ndiyo ilitufanya tuvumilie kuishi hapa na sijui nitaenda wapi na mke wangu huyu anayeumwa miaka mitatu sasa,” alisema Salehe.

Mkazi mwingine wa eneo hilo, Rashid Hamis alisema hawakuwa na taarifa kwamba nyumba zao zingebomolewa, hadi jana waliposhuhudia tingatinga likibomoa nyumba za jirani zao.

“Siyo kwamba hatujui kama eneo hili huwa linakumbwa na mafuriko ya mara kwa mara, tunafahamu sana ila ugumu wa maisha ndiyo unaotufanya tuendelee kuwepo. Wapo waliolipwa na wengine hatujalipwa kwa hiyo hatujui kwa kwenda,” alisema.

Wazee waliokumbwa na bomoaboa hiyo waliilalamikia Serikali kwa kutowapa taarifa mapema ili wajiandae.

“Nimekuja hapa tangu 1986, nimezaa watoto wote, na nilipata huduma zote ikiwemo umeme na maji. Kwani wakati Serikali inaleta haikujua kama hapa hapafai?

“Basi kama walijua tumevunja sheria, wangetuarifu mapema siyo kutushtukiza kiasi hiki,” alilalamika Mzee Juma Mwelomwe (73), mjumbe wa nyumba 10, katika Mtaa wa Hananasif.

Kwa wasio na uwezo kifedha walilazimika kukusanya vitu vyao na kuvitoa ili kupisha nyumba zibomolewe kisha kurejea tena na kuvihifadhi juu ya vifusi, wakitafakari hatua sehemu ya kuelekea.

Baadhi ya familia zilizobomolewa nyumba juzi ambazo hazikuwa na uwezo wa kuondoka, zilijihifadhi chini ya minazi, na kwenye vifusi vya nyumba zao zikisubiri neema ya kuhama.

“Nimelala hapahapa, nimempigia simu kaka yangu aliye Tabora ameahidi kuwa ataleta hela ili tupange walau chumba kimoja cha kujihifadhi,” alisema James Mbela akiwa na familia yake.

Hali halisi ya bonde la Msimbazi
Nyumba nyingi zilizobomolewa zilikuwa kwenye hali mbaya kutokana na kuathiriwa na mafuriko nyakati za mvua.

Njia za mitaa ya eneo hilo zilikuwa zimejaa maji machafu na hivyo kuwaweka katika hatari ya kukumbwa na ugonjwa wa kipindupindu.

Kutokana na ardhi yake kujaa maji, si rahisi eneo hilo kuwa na vyoo vya kudumu jambo linalochangia ugonjwa huo hatari kuwa sugu.

“Mvua ikinyesha huwa tunawakimbiza watoto, siku mbili tatu halafu tunarudi na kuendelea na maisha. Tutaenda wapi na hapa ndiyo tulizaliwa? Tumelizoea eneo hili,” alisema Chrostine Kibani, mkazi wa eneo hilo.

Serikali
Mkuu wa kitengo cha sheria wa NEMC, Manchale Heche alisema bomoabomoa hiyo itakayodumu kwa siku 30, itahusu nyumba 5,600 zilizojengwa kinyume cha sheria.

Heche alisema nyumba zaidi ya 500 zitavunjwa kwenye Bonde la Mto Msimbazi, ili kuwaepusha wakazi wa eneo hilo na hatari ya kukumbwa na mafuriko.

Alisema Serikali haiwezi kuwaacha watu wafe kwa mafuriko wakati uwezekano wa kuwaondoa upo.

“Ni mazingira machafu yasiyofaa kuishi binadamu. Hapa ndiyo chanzo cha mlipuko wa magonjwa ya kipindupindu, matumbo na hata malaria kwa sababu kuna maji mengi na machafu. Hakuna vyoo salama hapa kwa hiyo ni lazima tuwaondoe wananchi hawa hakuna njia nyingine,”alisema.

Kwa upande wake, Charles Mkalawa ambaye ni ofisa mipango miji wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, aliwataka wananchi kufuata sheria za ardhi badala ya kuvamia maeneo.

Wengine wachuma fedha
Wakati wapo waliokuwa wakiangua vilio, baadhi ya vijana na watoto waliitumia shughuli ya bomoabomoa kujiingizia kipato kwa kusomba mizigo, ili kuinusuru isivunjwe.

“Tangu jana nimeingiza zaidi ya Sh80,000 kwa sababu kila familia inayohitaji niifanyie kazi wananilipa Sh10,000 na siyo chini ya hapo. Mtaji wangu ni nguvu zangu mwenyewe,”alisema Kalim Sued, mkazi wa Magomeni.

Alisema hadi shughuli hiyo itakapomalizika, atakuwa amekusanya mpaka Sh200, 000 fedha ambayo hakuwahi kudhani angezipata kirahisi,

Mwananchi ilishuhudia watoto wakilipwa kati ya Sh200 hadi Sh500 kwa kazi hiyo.

Credits:Mwananchi


Mshirikishe na mwenzako kuhusu habari hii!!
BOMOA BOMOA: Nyumba zaidi ya 5000 kuvunjwa Dar!!! BOMOA BOMOA: Nyumba zaidi ya 5000 kuvunjwa Dar!!! Reviewed by Zero Degree on 12/19/2015 02:38:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.