Dar es salaam iko hatarini kukumbwa na mafuliko!!!
Mvua hizo zilizonyesha kwa takriban saa tatu tu, zimeathiri zaidi ya nyumba 200 za wakazi wa eneo la Tegeta Basihaya, Kinondoni.
Eneo hilo ni lile ambalo miezi saba iliyopita, Jakaya Kikwete akiwa Rais, aliiagiza Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kujenga mfereji ili kuruhusu maji yapite kwenye mkondo wake wa bahari bila kusababisha madhara kwa wananchi.
Katika maagizo hayo, pia Kikwete aliagiza nyumba zote zilizojengwa kwenye mkondo wa maji katika eneo hilo la Boko Basihaya zibomolewe na kujengwe mfereji mkubwa utakaowezesha maji kwenda baharini moja kwa moja.
Mafuriko ya wakati huo, yalitokana na mvua zilizonyesha kwa wiki mbili mfululizo na kusababisha vifo vya watu 12, huku mamia wakiyahama makazi yao.
Diwani wa kata hiyo, Michael Urio alisema jana kuwa licha ya kutumika kwa muda mfupi, daraja linalopokea maji yanayotoka kwenye eneo hilo na kuyatema upande wa pili limeanza kubomoka. Alisema Sh1.2 bilioni zilitumika kwa ujenzi wa mfereji huo.
Alisema maeneo mengi ya wananchi yamekumbwa na mafuriko hayo na kwamba, zinahitajika jitihada za haraka kuwanusuru kabla kasi ya mvua hizo haijaongezeka.
Akizungumza katika eneo la tukio, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee alisema ili kumaliza tatizo la mafuriko kwa wakazi wa Basihaya, Bunju na Tegeta lazima ujengwe mfereji mkubwa utakaogharimu zaidi ya Sh6 bilioni.
Mdee ambaye katika ziara yake ya kukagua maeneo yaliyokumbwa na mafuriko, aligongana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki na kuwaomba wataalamu wa Manispaa ya Kinondoni, kufanyia kazi suala hilo ili kuepusha madhara zaidi yanayoweza kujitokeza kwa wananchi.
Alisema mafuriko kwenye eneo hilo yamekuwa yakijirudia mara kwa mara na kwamba yanaweza kutatulika akisema walishatoa ushauri namna ya kukabiliana nayo.
Alisema ikiwa mvua hiyo itanyesha kwa mara nyingine, daraja linalopitisha maji hayo kumwaga upande wa pili wa Barabara ya Tegeta – Ununio linaweza kukatika na kufunga mawasiliano ya maeneo hayo.
Mkuu wa Mkoa aliwaagiza wataalamu wa manispaa hiyo; “kama maji yanaweza kutoka na kwenda kwenye mkondo wa bahari ni rahisi kufuatilia na kuona namna mfereji huo utakavyoweza kujengwa kwa uhakika.”
Kuhusu maji kujaa maeneo mbalimbali ya jiji, Sadiki alisema wanafuatilia kwa karibu maeneo mbalimbali ya jiji yenye matatizo sugu na kuyatafutia ufumbuzi huku akiwataka wanaoishi mabondeni kuondoka.
Wananchi walonga
Wakazi wa Basihaya na Boko, walisema hali bado ni tete kutokana na mfereji uliochimbwa kushindwa kukidhi wingi wa maji yanayopita kila mvua zinaponyesha na hivyo kusababisha mafuriko.
Mmoja wa wananchi hao, Enock Lucas alisema maji yalianza kufurika kwenye eneo hilo saa 1.30 asubuhi huku nyumba yake ikiwa miongoni mwa zilizokumbwa na mafuriko hayo.
“Tulijua mfereji uliojengwa kwa maagizo ya JK ungetosha kuondoa maji ya mkondo wa bahari ambayo kila mwaka yanafurika, tumeshangaa kuona maji yanaendelea kujaa kwa kasi na kuhatarisha maisha yetu huku mali na vitu vilivyokuwamo ndani vikiharibika,” alisema.
Mkazi mwingine wa Tegeta Pwani, Halima Athumani aliiomba Serikali kuwaondoa matajiri waliojenga nyumba na kuziba mifereji ya kupitisha maji, huku walalahoi wakihangaika.
“Kila mwaka tunanunua vifaa lakini vinakuja kuchukuliwa na mafuriko, maisha gani haya ya shida? Kama Serikali ipo itusaidie maana kuna waliojenga kwenye njia za maji,” alisema.
Mwenyekiti wa mtaa huo, Evod Rashid alisema: “Mvua ya saa tatu tu imesababisha zaidi ya nyumba 200 kukumbwa na mafuriko, sijui ikinyesha kwa siku mbili mfululizo hali itakuwaje? Nawaomba wataalamu watusaidie ili kunusuru uhai wetu, isitokee kama ilivyokuwa kipindi kile,” alisema Rashid.
Eneo la Tegeta-Block F
Akiwa Tegeta Block F, Sadiki alimuagiza mhandisi wa Manispaa ya Kinondoni kuifuatilia nyumba iliyojengwa kwenye mkondo wa maji kinyume cha sheria na kusababisha mafuriko kwenye mtaa huo ili ibomolewe.
“Kama tatizo ni mtu ametumia fedha zake kujenga nyumba kibabe na kuwasababisha wananchi madhara, ifuatiliwe na ikibainika ni kweli imejengwa kinyume cha utaratibu, ibomolewe ili tuwaepushe wananchi kukumbwa na mafuriko,” alisema.
Awali, wakazi wa eneo hilo, walisema mafuriko hayo yamesababishwa na mkazi mwenzao kujenga nyumba yake kwenye mkondo wa maji hivyo kuzuia maji kupita.
Waliilalamikia manispaa hiyo kwa kushindwa kutatua kero ya mafuriko kwenye eneo hilo iliyodumu kwa muda mrefu.
“Tumeshakwenda manispaa zaidi mara tano lakini hakuna suluhisho kwa sababu viwanja kwenye eneo la mkondo wa bahari vimegawiwa mwaka jana tu na tulianza kukumbwa na mafuriko katika msimu uliopita,” alisema mmoja wa wananchi hao, Rosemary Mwakitwange.
Mjumbe wa nyumba kumi wa mtaa huo, Mary Sinkara alisema wameishi eneo hilo kwa zaidi ya miaka 12 na hakukuwahi kuwa na mafuriko hadi pale nyumba hizo zilipojengwa.
“Tunataka Serikali isimamie uvunjwaji wa nyumba iliyozuia mkondo wa maji kushindwa kupita kwenye eneo hilo na kutusababishia hasara kubwa kutokana na mafuriko. Hali ni mbaya kwa sababu maji yamejaa kiasi kwamba hatuwezi kufanya shughuli nyingine,” alisema.
Credits: Mwananchi
Mshirikishe na mwenako kuhusu habari hii!!
Dar es salaam iko hatarini kukumbwa na mafuliko!!!
Reviewed by Zero Degree
on
12/16/2015 11:52:00 AM
Rating: