Dar es salaam: Majambazi yaua walinzi wawili, na kupora katika benki mbili tofauti!!
Hilo ni tukio la pili kutokea katika kipindi cha siku nane, baada wiki iliyopita majambazi manne kupora fedha zinazokadiriwa kufikia Sh70 milioni, eneo la Tazara karibu na ofisi ya Shirika la Taifa la Utangazaji (TBC).
Tukio hilo la aina yake lilitokea jana kati ya saa tisa alasiri na saa 10 jioni katika eneo la Chanika kwenye Manispaa ya Ilala. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala, Lucas Mkondya alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kwamba, mbali na kuua pia majambazi hayo yaliwajeruhi watu wengine wanne.
“Majeruhi hawa bado wanaendelea kupata matibabu, huku polisi ikiendelea na msako wa kuwatafuta majambazi hao,” alisema Mkondya.
Kamanda huyo alisema, majambazi hayo yaliingia katika Benki za CRDB na DCB na kupora fedha zote zilizokuwa eneo la kaunta kisha kutokomea nazo.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Mohamed Khalfan aliliambia Mwananchi kwamba majambazi hayo yalifika katika benki hizo yakiwa yamepakizana kwenye pikipiki nne aina ya boxer.
Aliongeza kuwa baada ya kushuka katika pikipiki hizo, yalijigawa katika makundi kisha kwenda moja kwa moja katika benki hizo zilizopo Mtaa wa Chanika kwa Ngwale.
“Kabla ya kuingia ndani walianza kuwamininia risasi walinzi wa benki waliokuwa nje ambao ni wale wa Suma JKT. Baada ya hapo waliingia ndani ya benki hizo,” alisema Khalfan.
Alisema baada ya kuchukua fedha hizo katika mabegi, yaliondoka nazo yakitangulia mawili na mengine yalifuatia nyuma yakiondoka kwa kasi.
Alipotafutwa baadaye jana usiku kuzungumzia kiasi cha fedha zilizoporwa, Mkuu wa Operesheni wa Kanda Maalumu ya Polisi, Simon Siro aliyekuwa eneo la tukio alisema Kamishna wa Kanda hiyo, Suleiman Kova atalitolea maelezo suala hilo.
Hata hivyo, Kova alipopigiwa simu yake, ilipokewa na mtu aliyejitambulisha kuwa ni msaidizi wake akisema kuwa bosi wake yuko kwenye chopa na akishuka atamfikishia taarifa. Taarifa zaidi kuhusu fedha zilizoporwa zitatolewa baadaye alisema Mkondya.
Creidts: Mwananchi
Mshirikishe na mwenzako kuhusiana na habari hii!!
Dar es salaam: Majambazi yaua walinzi wawili, na kupora katika benki mbili tofauti!!
Reviewed by Zero Degree
on
12/09/2015 03:01:00 PM
Rating: