Loading...

Kiwanda cha MBAO kunufaisha Wakazi 250 Iringa.


Iringa. Wakazi 250 wa Kijiji cha Ugwachanya, Kata ya Mseke wilayani hapa Mkoa wa Iringa, wanatarajia kunufaika na ajira zitakazotolewa na kiwanda cha kuweka dawa kwenye nguzo za umeme kitakapoanza kazi.

Ajira hizo zitatolewa na kiwanda hicho cha Agora Wood Products kitakachokuwa kinaweka dawa kwenye nguzo 200 kwa siku.

Ofisa Mtendaji wa kampuni hiyo, Elisha Msengi alisema, watatumia teknolojia mpya kuwezesha dawa kupenya hadi ndani ya nguzo na bidhaa zingine zinazotokana na miti, hivyo kuongeza ubora na matumizi ya muda mrefu ya bidhaa hizo.

“Kitakapokamilika kiwanda kitatoa ajira za moja kwa moja zaidi ya 50 na nyingine 200 zisizo za moja kwa moja,” alisema na kuongeza kwamba, kiwanda hicho kitachangia kwa kiwango kikubwa mapato ya fedha za halmashauri na Serikali kuu kwa kulipa kodi na tozo muhimu.

Alisema ujenzi wa majengo na miundombinu iliyopo katika kiwanda hicho ulianza Septemba 2015 ukihusisha ununuzi wa mitambo, ardhi, malighafi za ujenzi na kazi kwa zaidi ya Sh500 milioni ambazo zilichangwa na vijana hao.

Msengi alisema hadi kukamilika kwake, kiwanda hicho kitagharimu zaidi ya Sh2.5 bilioni. Hata hivyo, alionyesha kushangazwa jinsi mradi huo wenye manufaa makubwa kwa mkoa na Taifa ulivyokosa mkopo katika moja ya benki za nchini na kulazimu kusubiri kwa miezi tisa tangu uombwe.

Akiweka jiwe la msingi katika kiwanda hicho, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alisema, ni faraja kujengwa na kumilikiwa na wazawa kwa asilimia 100.

Masenza alisema Serikali ya Awamu ya Tano imelenga kuigeuza Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa viwanda ili badala ya kuuza malighafi, ziuzwe bidhaa ambazo zimetengenezwa kwa ubora na zenye thamani katika soko la ndani na nje ya nchi.


Credits: Mwananchi

Comment & Share this story!!
Kiwanda cha MBAO kunufaisha Wakazi 250 Iringa. Kiwanda cha MBAO kunufaisha Wakazi 250 Iringa. Reviewed by Zero Degree on 12/29/2015 01:22:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.