Loading...

Lukuvi atangaza kiama kwa vigogo waliokiuka sheria na kujenga katika fukwe za bahari!!!


WAKATI zoezi la kutumbua majipu likiendelea kufanya kazi katika maeneo mbalimbali, safari hii kiama kinaelekea kuyakuta mahekalu ya vigogo yaliyojengwa kwa bei mbaya katika fukwe za Bahari ya Hindi jijini Dar es Salaam, Risasi Mchanganyiko linaripoti.


Kwa mujibu wa duru za mazingira na kwenye Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, baada ya kuzidiwa na nguvu ya fedha kwa muda mrefu, majumba hayo yatabomolewa wakati wowote kuanzia sasa kwa kuzingatia sheria zinazolinda mazingira pamoja na katazo la kujenga maeneo ya hifadhi na wazi.




Moja ya mjengo huo ulioko ufukweni.



KUTOKA WIZARA YA ARDHI


Kwa mujibu wa ripoti kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, watu wengi wamejenga katika maeneo ya wazi yaliyokuwa yametengwa kwa sababu maalum, katika hifadhi ya miti aina ya mikoko kandokando ya bahari pamoja na umbali ambao hauruhusiwi kisheria.



…..Muonekano wa mjengo mwingine pembezoni mwa bahari ya Hindi.

“Kwa mujibu wa sheria, mtu yeyote haruhusiwi kujenga ndani ya mita 60 kutoka usawa wa bahari au mita 30 kutoka kwenye mto. Katika maeneo hayo, nyumba nyingi zitabomolewa katika mikoa ya Mtwara, Lindi, Dar es Salaam, Pwani na Tanga ambazo zimejengwa kandokando ya bahari na mito.

Na ubomoaji huu hautakuwa na fidia labda kama nyumba hizo zilijengwa kabla ya kupitishwa kwa sheria hii mwaka 1992,” kinasema chanzo kutoka wizarani kinachoomba hifadhi ya jina lake.

Chanzo hicho kinamnukuu aliyekuwa Waziri wa Wizara hiyo, Anna Tibaijuka aliyesema kuwa serikali inatambua kuwepo kwa nyumba 300 tu zenye hati halali, ambazo zilijengwa pembezoni mwa fukwe hizo kabla ya sheria hiyo kupitishwa, ambazo hata hivyo, zitabomolewa baada ya maridhiano baina ya pande mbili, kwani kiasili, makazi karibu na bahari au mito ni hatari kwa maisha ya binadamu.

WIZARA YA MAKAMU WA RAIS NAYO

Wizara ya Makamu wa Rais inayoshughulikia mazingira, inasema kuwa wakati serikali ilipopiga picha kwa ‘satelite’ mwaka 2005 katika mto Ndumbwi unaoingiza maji katika bahari ya Hindi eneo la Mbezi Beach, pembeni yake palionekana pakiwa wazi bila nyumba yoyote, lakini hivi sasa umevamiwa kiasi cha kushangaza.



Wizara hiyo ilisema ilikuwa imeanzisha utaratibu wa kufanya ukaguzi wa nyumba zilizojengwa kinyume cha sheria sambamba na ubomoaji wake, ili kuhakikisha sheria zinazingatiwa na watu wote.

LUKUVI AWATOLEA UVIVU VIGOGO

Hata hivyo, wakati wananchi hasa wa hali ya chini wakiamini vigogo waliojenga kandokando ya bahari na mito hawawezi kufanywa lolote kwa uwezo wao kifedha, Waziri aliyerejeshwa katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wiliam Lukuvi ameweka wazi kuwa nguvu alizonazo hivi sasa, hazizuiliki.

Akizungumza wakati wa hafla ya kuwaapisha mawaziri wa baraza jipya ikulu jijini Dar es Salaam wiki iliyopita, Lukuvi alisema wakati wa matajiri kufanya wanavyotaka umepita na kwamba safari hii, licha ya kutaka sheria kuchukua mkondo wake katika ujenzi wa maeneo ya ufukweni, pia wakati wa matajiri kuwaonea wanyonge na kuwadhulumu ardhi umefikia mwisho wake.

“Nina nguvu mpya, watu wote waliokiuka sheria kwa kuvamia maeneo ya wazi, kwenye fukwe na ukiukwaji mwingine, kubomoa wenyewe kabla sijawafikia. Kama wasipoondoka wenyewe nitawaondoa maana sasa nina rungu,” Waziri Lukuvi alisema.


MAKONDA NAYE AMUUNGA MKONO

Akizungumzia suala hilo juzi, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda, alisema atakuwa bega kwa bega na Waziri Lukuvi katika kuhakikisha sheria zinafuatwa na wote waliojenga kinyume cha sheria wanaondolewa bila kujali majina na nyadhifa zao.

“Tutakachofanya ni kuhakikisha sheria zilizopo zinafuatwa na kila mtu, tunataka kwenda na kasi ya rais Magufuli kwa sababu anataka watanzania waishi kwa usawa, haiwezekani mtu avunje sheria halafu aachwe wakati wengine wanawajibishwa,” alisema na kuongeza kuwa nyumba zote zilizojengwa pasipo kufuata utaratibu uliopo lazima zibomolewe.


WAMILIKI WAHAHA, WAKOSA PA KWENDA

Wakati viongozi wa serikali wakiapa kuzivunja nyumba hizo, wamiliki wake wameelezwa kuhaha wasijue la kufanya, hasa kutokana na ‘usiriaz’ wa rais Dk. John Magufuli katika kufuata sheria.

“Tokea tangazo la Waziri Lukuvi kuhusu bomoa bomoa ya nyumba zao, wamiliki wanahaha kwelikweli, huku hakukaliki, wanahangaika kupiga simu kwa watu wao ili wawasaidie, lakini kila mmoja anakataa kwa sababu hataki kuingia mikononi mwa Magufuli,” alisema mtu mmoja mwenye nyumba pembezoni mwa barabara ya Kawe.

Ufukwe wa Kawe ni miongoni mwa eneo lililovamiwa kwa wingi na matajiri waliojenga majengo ya kifahari, hasa karibu na sehemu ya uhifadhi wa miti ya Mikoko.



“Jamaa walizoea zamani wakija watu wa Manispaa wanapiga simu sijui wapi, ghafla wale watu nao wanapigiwa simu waache zoezi, sasa baada ya Magufuli kuifumua bandari na TRA, watu wamekuwa waoga, hawana uhakika kama simu zao zitafanya kazi, wamebakia kusubiri kuona kitakachotokea,” alisema mtu huyo aliyejitambulisha kama Aidan!


Credits: Global publishers



Mshirikishe na mwenzako kuhusu habari hii!!
Lukuvi atangaza kiama kwa vigogo waliokiuka sheria na kujenga katika fukwe za bahari!!! Lukuvi atangaza kiama kwa vigogo waliokiuka sheria na kujenga katika fukwe za bahari!!! Reviewed by Zero Degree on 12/16/2015 10:16:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.