Loading...

Moshi: Jeshi la polisi mkoani kilimanjaro labaini kiwanda 'FEKI' cha pombe aina ya KONYAGI!!!


Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, limewatia mbaroni watu watano kwa tuhuma za kutengeneza pombe kali bandia aina ya Konyagi.


Kukamatwa kwa watu hao kumekuja huku kukiwa na taarifa za kuzagaa kwa pombe za aina hiyo zinazotengenezwa nchini na nchi jirani na kuwekwa katika chupa halisi.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa Kilimanjaro, Fulgence Ngonyani aliliambia gazeti hili jana kuwa, watuhumiwa hao walikamatwa wakitengeneza Konyagi kubwa bandia katoni 186, ndogo na za viroba katoni 93.

Ngonyani alisema watuhumiwa hao, mafundi magari wawili, mkulima, mwendesha bodaboda na mfanyabiashara, walikamatwa wakitengeneza pombe hizo katika nyumba iliyopo mjini Moshi.

Alisema juzi saa 9:30 alasiri, polisi walipokea taarifa kutoka kwa raia mwema kuwa kuna watu wanatengeneza pombe hiyo kienyeji katika eneo la Shah Tours Sango Manispaa ya Moshi.

“Polisi walikwenda eneo hilo na walipowafanyia upekuzi waliwakuta ndani ya nyumba ambayo mmiliki wake bado hajafahamika wakiwa wanaendelea kutengeneza pombe hiyo,” alisema.

Kamanda huyo ametoa hadhari kwa wananchi kuwa makini na pindi wanapobaini kuwapo watu wanaozalisha pombe za bandia watoe taarifa mamlaka zinazohusika, ikiwamo polisi.

Mwanasayansi mtafiti wa zamani katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Profesa Watoky Nkya alisema pombe bandia zinaweza kumsababishia mnywaji upofu na kuathiri ini na figo.

Profesa Nkya alisema viwanda vingi vya mitaani vinavyozalisha pombe hizo bandia havina mashine zinazotenganisha kati ya ethanol na methanol, hivyo pombe kuwa na kemikali zote mbili.

“Ethanol haina madhara, lakini methanol ni sumu ina athari kubwa, mashine hizi za mitaani mara nyingine zinashindwa kutenganisha ethanol na methanol,” alisema.

Profesa Nkya alisema watengenezaji wa pombe hizo wamekuwa wakiweka rangi ili zifanane na pombe halisi na wakati mwingine rangi wanazozitumia huwa na madhara kwa mnywaji. Alisema utengenezaji huo wa pombe kienyeji unapaswa kudhibitiwa haraka iwezekanavyo.




Credits: Mwananchi


Mshirikishe na mwenzako kuhusu habari hii!!
Moshi: Jeshi la polisi mkoani kilimanjaro labaini kiwanda 'FEKI' cha pombe aina ya KONYAGI!!! Moshi: Jeshi la polisi mkoani kilimanjaro labaini kiwanda 'FEKI' cha pombe aina ya KONYAGI!!! Reviewed by Zero Degree on 12/23/2015 07:23:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.