Bodaboda Zinazopandisha ‘Mishikaki’ Kupigwa Picha
Jeshi hilo litatumia mbinu hiyo ili kuepusha ukamataji kwa kuwakimbiza wale wanaofanya hivyo kwa lengo la kuepuka kusababisha ajali wakati wa kuwakamata madereva hao wanaobeba mshikaki.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha, Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Bonaventura Mushongi alisema kuwa mbinu hiyo itasaidia kuwabaini na kuwapiga faini kwa mujibu wa sheria.
“Tumeona tufanye hivyo kwani ukamataji wa zamani wa kufukuzana siyo mzuri, unaweza ukasababisha ajali kwa wanaotumia pikipiki hiyo na hata kugonga watu au mali katika kukwepa mkono wa sheria lakini kwa kuwapiga picha tutawatafuta na kuwakamata wakiwa hawana abiria,”alisema.
Alisema mbali ya kukamata madereva bodaboda wanaobeba mshikaki ambayo ni kinyume cha sheria, pia watawakamata kwa makosa mengine kama vile leseni, kutokuwa na kofia mbili ngumu na kutozingatia sheria za uendeshaji na usalama barabarani.
“Pia tunawaomba waendesha bodaboda watupe ushirikiano katika kubaini wahalifu ambao wamekuwa wakitumia usafiri huo kufanikisha wizi hivyo wanapaswa kutupa taarifa za watu wanaopanga kwenda kufanya uhalifu kutumia vyombo hivyo,” alisema Mushongi.
Aidha alisema kuwa endapo madereva hao wa bodaboda watatoa ushirikiano kwa polisi itasaidia sana kukabiliana na uhalifu ambao umekuwa ukijitokeza mara kwa mara.
“Pia kuna taarifa kuwa baadhi ya waendesha bodaboda nao wanajihusisha na uhalifu, tunawataka waache vitendo hivyo kwani wao ni watoa huduma na endapo watabainika kufanya hivyo watakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria,” alisema Mushongi.
Alibainisha kuwa jeshi lake litashirikiana na viongozi wa bodaboda katika kuhakikisha kuwa wanafuata sheria na kupambana na uhalifu na siyo wao kuwa chanzo cha uhalifu na kuvunja sheria.
ZeroDegree.
Bodaboda Zinazopandisha ‘Mishikaki’ Kupigwa Picha
Reviewed by Zero Degree
on
1/20/2016 10:12:00 AM
Rating: