Loading...

Wizara, taasisi, idara zaandaliwa kibano cha sera.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala bora), Angellah Kairuki.

Dodoma. Serikali iko mbioni kupeleka bungeni muswada wa sera ya Serikali mtandao ili kuzibana taasisi na wizara kuingia katika mfumo huo.



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala bora), Angellah Kairuki alitoa kauli hiyo wakati akifungua mafunzo kwa maofisa wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) wa taasisi za Serikali katika ukumbi wa UCC mjini hapa leo.

Kairuki alisema sera hiyo inatarajia kukamilika mwaka huu wa fedha kwa kuwa ni muhimu, kwani itaisaidia Serikali katika kubana matumizi.

Alisema katika mpango huo ni lazima kuangalia matumizi ya tovuti ndani ya Serikali ili iweze kuleta tija na mabadiliko yaliyotarajiwa.

“Hata hivyo nasisitiza juu matumizi hayo na ninaziomba taasisi zingine kuanza kutumia Tehama ili kupunguza gharama za mikutano na vikao. Sisi ofisi yetu tulishaanza na tumeunganishwa na sekretarieti za mikoa, na mikutano na maagizo yetu yanafika kwa wakati,” alisema Waziri huyo aliitaja mikoa ambayo bado haijafikiwa na mfumo huo kuwa ni Njombe, Simiyu na Geita.

Pia, aliagiza watumishi wote wenye anuani za baruapepe kuanzia sasa waanze kuzitumia badala ya anuani zao binafsi wakati wakifanya mawasiliano ya kiserikali.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Serikali Mtandao, Dk Jabil Bakari alisema mafunzo hayo ambayo yanatarajiwa kumalizika Juni 3, mwaka huu yanahudhuriwa na maofisa wa Tehama 210.

Dk Bakari alisema nia ya Serikali ni kuona jinsi inavyoweza kuboresha mifumo ya ndani ya mawasiliano, hususan kwa watumishi wake.

Alisema katika awamu ya kwanza watumishi 20 kutoka taasisi 17 walikuwa wakiendelea na mafunzo mjini Dodoma, ilhali jijini Dar es Salaam kulikuwa na watumishi 30 kutoka taasisi 23.

Mkurugenzi wa Tehama wa Serikali, Priscus Kiwango alisema katika mafunzo hayo wanaangalia mifumo ya mawasiliano ikiwamo mpango wa ufuatiliaji elimu na Tehama yenyewe.

Alisema lengo la kufanya hivyo ni kutafuta tija katika utendaji kazi wa idara na wizara za Serikali kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.



ZeroDegree.
Wizara, taasisi, idara zaandaliwa kibano cha sera. Wizara, taasisi, idara zaandaliwa kibano cha sera. Reviewed by Zero Degree on 1/19/2016 10:27:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.