Loading...

BOMOABOMOA Dar yapigwa 'STOP' mahakamani.


Wakazi wanaoishi maeneo hatarishi ya mabondeni katika Jiji la Dar es Salaam, wakimbeba mwanaharakati na mtetezi wao, Msafiri Angalienimpendu baada ya Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi kutoa uamuzi wa kusitisha ubomoaji wa baadhi ya nyumba zao, wakati wakisubiri kufungua kesi ya msingi.

Wakati NEMC ikianza tena ubomoaji wa nyumba zilizoko kwenye maeneo ya mabondeni, Mahakama Kuu imeifunga mikono Serikali kwa muda kuendelea na operesheni hiyo kwa wakazi 674 waliofungua kesi kupinga bomoabomoa.

Uamuzi huo wa Mahakama Kuu utahusu nyumba za wakazi hao tu, lakini Baraza la Usimamizi wa

Mazingira (NEMC) linaloendesha ubomoaji huo, litalazimika kufanya kazi ya ziada kutambua nyumba za wanaohusika na amri hiyo kutokana na majina yao kutojulikana hadi wakati amri hiyo ikitolewa.

Wilayani Temeke, wananchi walimpeleka mbunge wao hadi eneo la Keko na kumuonyesha jengo linaloziba barabara tatu, wakisema operesheni hiyo itakapowafikia, ianze na jengo hilo walilosema ni kero kwa wakazi wa Keko, Chang’ombe na sehemu nyingine waliokuwa wanatumia barabara hizo.

NEMC ilisitisha operesheni ya ubomoaji nyumba zilizojengwa kwenye maeneo ya wazi, fukwe, kingo za mito na mabondeni na kutoa siku 14 kwa wakazi kuhamisha vifaa vyao na kubomoa nyumba. Muda huo ulimalizika jana na kazi hiyo ilianza tena bila ya kuwapo vikwazo kutoka kwa wananchi kama ilivyokuwa mwanzoni.

Lakini wakazi saba waliofungua kesi kwa niaba ya wenzao zaidi ya 670, walikuwa wameelekeza nguvu kwenye vyombo vya sheria, kupinga kubomolewa nyumba bila ya kuonyeshwa makazi mbadala huku wakiomba mahakama kutoa amri ya kuzuia ubomoaji hadi hapo shauri lao litakapoamuliwa.

Maombi hayo ya Ali Kondo Mshindo na wenzake sita katika kesi hiyo inayosikilizwa Kitengo cha Ardhi cha Mahakama Kuu yalitolewa uamuzi jana.

“Nimeridhika kuwa katika shauri hili kwa misingi ya haki, utawala bora na sheria kuna watu wanastahili haki ya kusikilizwa kutoa hoja zao kwa nini wanataka kufungua kesi kwa niaba ya wenzao,” alisema Jaji Penterine Kente anayesikiliza kesi hiyo baada ya mawakili wa pande zote mbili kutoa hoja zao.

“Lakini kwa kuwa uvunjaji wa nyumba zao unaweza kuendelea, nimeona kuna sababu ya msingi ya kutoa amri ya zuio kwa wajibu maombi wasimamishe ubomoaji kusubiri kusikilizwa kwa maombi namba 822,” aliongeza.

Jaji Kente alisema amri hiyo ya zuio itawahusu wakazi ambao wanahusika na kesi hiyo tu na kwamba ubomoaji na uwekaji alama za X unaweza kuendelea kwa wasiohusika.

“Katika kuondoa mashaka, amri hii ya mahakama inawahusu wale tu walioko katika kesi. Hivyo Serikali haizuiwi kuendelea na zoezi la utambuzi, uwekaji alama na ikiwezekana hata ubomoaji wa nyumba katika maeneo mengine ambako hawahusiki katika kesi hii,” alisema Jaji Kente na kuongeza:

“Wakili (anayewatetea watoa maombi, Abubakar) Salim awasilishe mahakamani leo hii orodha ya majina na anuani za makazi ya wale wote watakaohusika katika kesi itakayofunguliwa, ili zuio la kutovunjwa kwa nyumba zao litekelezwe kwa urahisi.”

Baada ya kusoma uamuzi huo Jaji Kente aliahirisha shauri hilo hadi Jumatatu wakati maombi hayo ya kibali yatatajwa kwa ajili ya kupanga tarehe ya kuyasikiliza.

Wajibu maombi katika shauri hilo ambao ni Manispaa ya Kinondoni, NEMC na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), wametakiwa kuwasilisha mahakamani hapo hati ya kiapo kinzani keshokutwa.

Operesheni ya bomoabomoa ilianza Desemba mwaka jana kwa watu waliojenga bonde la Mto Msimbazi eneo la Mkwajuni na Magomeni kabla ya kuendelea na maeneo mengine, lakini ilisitishwa kwa muda Desemba 22 hadi Januari 5, mwaka huu.

Lakini kabla ya muda huo wa siku 14, Desemba 28 wananchi hao walifungua kesi kupinga ubomoaji huo.

Hoja za mawakili
Juzi wakati wa usikilizwaji wa maombi hayo, mawakili wa wajibu maombi, Balton Mahenge wa Manispaa na Wakili wa Serikali Mkuu (PSA), Gabriel Malata anayewakilisha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu na Nemc waliomba muda wa kuwasilisha hati ya kiapo kinzani ili waweze kujibu vizuri hoja za wananchi hao.

Kutokana na kuomba muda huo, wakili wa wananchi hao aliiomba mahakama iamuru hali iendelee kuwa kama ilivyokuwa wakati shauri lao lilipowasilishwa mahakamani, akimaanisha ubomoaji uendelee kusitishwa na wananchi waendelee kuishi kwenye nyumba hizo hadi mahakama itakapotoa uamuzi.

Lakini hoja hiyo ilipingwa na upande wa Serikali uliodai kuwa waombaji hawakuwa na sifa kwa kuwa shauri lao bado halijatambuliki mahakamani kutokana na maombi yaliyoko mahakamani ni ya kibali cha kufungua kesi ya uwakilishi na yalikuwa hayajasikilizwa na kupewa hicho kibali cha kufungua kesi.

Akijibu pingamizi hilo, wakili wa wananchi hao alisema wanaomba nyumba zao zisibomolewe, ili kusubiri usikilizwaji na uamuzi wa maombi ya kufungua kesi ya uwakilishi kupinga ubomoaji na wanalazimika kuomba kibali kwa kuwa watu wote watakaothirika na hatua za Serikali, wana maslahi sawa na kwa hali ya mazingira ya mahakama hawawezi wote kwenda mahakamani badala yake kwa kuwakilishwa.



Bomoabomoa yaanza tena

Wakati kesi hiyo ikisikilizwa katikati ya jiji, ubomoaji ulianza tena jana saa 3:20 asubuhi maeneo ya Hananasif na Suna wilayani Kinondoni ambako historia ya ya baadhi ya nyumba takriban miaka 40 ilifikia ukingoni.

Maofisa wa NEMC walifika na matingatinga mawili katika mitaa hiyo na kubomoa nyumba zilizowekwa alama ya X.

Tofauti na ubomoaji wa awali, operesheni ya jana haikuwa na upinzani wowote kutoka kwa wananchi wengi wao kuondoa mali zao na wengine kuendelea na kazi hiyo ya kuhamisha na kubomoa madirisha na milango kwenye nyumba zao kabla tingatinga halijawafikia.

“Tumemchagua wenyewe, tunabomoa wenyewe wacha tuisome namba, bomoa bomoa mbele kwa mbele,” waliimba wakazi hao wakibadili maneno ya wimbo maarufu wa kampeni za chama tawala unaoitwa “CCM Mbele kwa Mbele”.

“Kama wanataka kuja kutuvunjia waje tu. Hata tukisema tuondoke hapa, hatujui pa kuelekea. Hawa unaowaona wanaondoka kwa kutumia usafiri wa mafuso ni wapangaji siyo wenye nyumba,” alisema Salum Utari, mkazi wa eneo hilo akiwa mbele ya nyumba yake.

Utari alimtaka Rais John Magufuli kujitokeza hadharani na kutoa tamko juu ya sakata hilo la bomoabomoa kwa kuwa linakwenda kinyume na ahadi zake kwa Watanzania.

“Wakati wa kampeni, Mheshimiwa (Magufuli) aliahidi kuwa atakuwa bega kwa bega na wanyonge. Kwa sakata hili la kutubomolea nyumba ni sawa na kututoa kwenye umasikini kutupeleka kwenye ufukara,” alisema Utari aliyetaka Rais awaeleze wananchi watapelekwa eneo gani.

Baadhi ya wakazi walioanza kuhama wamekiri kuwa eneo hilo ni hatarishi na kuomba msaada wa kusafirisha mali zao na wengine fedha za kuwawezesha kuanzia kupanga vyumba maeneo mengine. “Nilianza kutoa mali zangu tangu wiki mbili zilizopita, lakini ni nusu tu nimefaulu kuzipeleka Bagamoyo. Sina fedha, nimeishiwa. Watoto wangu kama hivi shule zimefunguliwa hawajui hatima yao inabidi niwahamishie Kelege, Bagamoyo sababu maisha ya hapa siyawezi tena,” alisema George Mkondoa.

Mkondoa mwenye mke na watoto wawili, alisema kwa majuma mawili amekuwa akilala kwenye kibanda alichojenga kwa mabati karibu na barabara ya Kawawa ili kulinda mali zake, lakini akipata msaada wa usafiri, ataondoka.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Suna, Salum Hamis alisema wamelazimika kuhama ili kusalimisha baadhi ya mali walizozitolea jasho na si kutokana na agizo la Serikali.

“Walituambia tusipotoa vitu vyetu, watatuvunjia. Kwa hiyo waache propaganda kuwa tumebomoa wenyewe. Hapa sisi tumeamua kufanya hivi kuokoa mali zetu,” alisema Hamis na kuongeza: “Eneo hili lina nyumba 900. Kila nyumba moja ina kaya saba, wingi huu wa kuishi hapa unatokana na hali zao za maisha, si bure.”

Hata hivyo, hali ilikuwa tofauti kwa wakazi wa Jangwani, ambako baadhi ya wakazi walionekana kutokuwa na wasiwasi.

Mwanasheria wa NEMC, Heche Suguti alisema operesheni hiyo itaendelea hadi Gongo la Mboto na kuwahimiza wanaoweka alama kuendelea kutoa mali zao.

Wilayani Temeke, wananchi waliamua kutumbua jipu kabla ya ubomoaji haujawafikia.

Wakazi zaidi ya 200 wa Keko Chang’ombe walimtaka Mbunge wa Temeke, Abdallah Mtolea kuishinikiza Serikali kubomoa jengo lililoziba barabara tatu na ambalo liko juu ya bomba la maji safi la Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (Dawasco).

Akizungumza kwa niaba ya wenzake mbele ya mbunge huyo, Dallas Msowoya alisema barabara tatu za Toroli, Mizani na Tameco zimezibwa na jengo hilo.

Msowoya alisema kabla ya kujengwa, eneo hilo lilikuwa na mizani ya Shirika la Usagishaji la Taifa (NMC). Imeandikwa na James Magai, Raymond Kaminyoge, Nuzulack Dausen na Bakari Kiango.


Source: Mwananchi

Comment & Share this!!
BOMOABOMOA Dar yapigwa 'STOP' mahakamani. BOMOABOMOA Dar yapigwa 'STOP' mahakamani. Reviewed by Zero Degree on 1/06/2016 11:58:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.