Loading...

Watu 1,500 wakumbwa na mafuriko Morogoro.


Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema) Mkoa wa Morogoro, Devotha Minja, akiongozwa na Diwani wa Kata ya Magomeni, Abdallah Uweli kutembelea maeneo yaliyokumbwa na mafuriko katika Kitongoji cha Mbwamaji wilayani Kilosa jana baada ya Mto Mkondoa kubomoka.


Kilosa. Zaidi ya wakazi 1,500 wa kaya 250 katika Kitongoji cha Mbwamaji wilayani hapa Mkoa wa Morogoro, wamekumbwa na mafuriko baada ya mvua kubwa kunyesha na kusababisha hasara ya vitu mbalimbali, ikiwamo nyumba kubomoka na uharibifu wa mali.

Mafuriko hayo licha ya kuharibu mali za kata hizo, pia yameharibu miundombinu ya barabara ya Mikumi hadi Kilosa na mazao ya aina mbalimbali katika mashamba yanayokadiliwa kufikia ekari 400.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mbwamaji, Abdallah Songoro (51) alimueleza Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Devotha Minja kuwa mafuriko hayo yamesababisha uhaba wa vyakula.

Songoro alisema mafuriko hayo yalianza kuingia katika makazi ya watu saa sita usiku juzi hadi jana saa tano asubuhi, baada ya kupasua kingo za Mto Mkondoa katika eneo la shamba la Magereza.

“Waathirika wote katika mafuriko haya wengi wao wanaishi katika majengo ya Mahakama ya Mwanzo, Shule ya Msingi Magomeni na jengo la boma la ofisi ya ofisa mtendaji wa kata na mpaka sasa hivi bado hatujapata taarifa ya kifo,”alisema Songoro.

Kwa upande wake, Minja aliyewatembelea wahanga hao baada ya kukagua eneo lililokumbwa na mafuriko, alisema Serikali inapaswa kutoa huduma za dharura haraka ili kaya hizo ziendelee na maisha yao.

“Nawapeni pole kwa tukio lililotokea, lakini kutokana na hali halisi nawaombeni msirudi tena kwa wale wenye nyumba ambazo hazijabomoka, kwani mvua inaweza kunyesha tena na kusababisha maafa,” alisema.

Mmoja wa waathirika hao, Jema Mduwile (25) alisema mafuriko hayo yalivamia katika makazi yao wakati wamelala na kazi ya kuwaokoa watoto ilikuwa ngumu kutokana na kasi ya maji. “Nilifanikiwa kuwaokoa watoto wangu wote wanne kwa kuwabeba kutoka ndani ya nyumba hadi sehemu salama, namshukuru Mungu kwani maji yaliingia ndani wa kasi na kufikia usawa wa madirisha,” alisema.




Source:Mwananchi

Comment & Share this!!
Watu 1,500 wakumbwa na mafuriko Morogoro. Watu 1,500 wakumbwa na mafuriko Morogoro. Reviewed by Zero Degree on 1/06/2016 12:03:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.