Loading...

Burundi sasa yajadiliwa kimyakimya.


Arusha. Mazungumzo ya kutafuta suluhu ya mgogoro wa nchi ya Burundi yameanza jijini Arusha bila Serikali ya nchi hiyo kutuma wawakilishi kwenye mkutano huo.


Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kanda na Ushirikiano wa kimataifa, Dk Augustino Mahiga alisema juzi kwenye makao makuu ya EAC kuwa, Serikali ya Burundi imeomba kikao hicho kusogezwa mbele kutokana na sababu mbalimbali.

Viongozi wengine waliohudhuria mkutano huo ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Nchi za Maziwa Makuu (ICGLR), Georges Chicoti, Waziri wa Ulinzi wa Uganda, Crispus Kionga ambaye ni mwakilishi wa mpatanishi wa mgogoro huo na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Dk Richard Sezibera.

“Mkutano huu ni kuileza dunia kuwa, tumejitolea kuhakikisha tunashirikiana na Burundi kutafuta amani,” alisema Dk Mahiga. Alisema kutokana na mkutano huo kukosa wawakilishi wa Burundi, mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliokua ufanyike Januari 8, jijini Arusha ulisogezwa mbele kwa kuwa mkutano huo wa juzi ndiyo ungejadili mapendekezo ya mkutano wa juzi. Alisema Burundi haipingi mazungumzo taarifa zilizopo ni kuwa, bado inajiandaa kwa ajili ya mazungumzo hayo, na kutofika kwa ujumbe wa Serikali kwenye mazungumzo ya Arusha siyo ushahidi kuwa, Rais Pierre Nkurunziza anapinga juhudi za upatanishi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na nchi nyingine.

Chama tawala cha Burundi juzi kilitoa wito wa kuwapo kwa ushirikiano wa karibu kati ya Uganda ambayo ni mpatanishi wa mazungumzo ya kutafuta amani na kamati ya mazungumzo ya kitaifa ya Burundi CNDI.

Msemaji wa chama tawala cha Burundi CNDD-FDD, Danile Ndabirabe alisema CNDI inatakiwa kuwa ni utaratibu pekee wa kisheria unaotakiwa kuandaa, kuratibu na kutekeleza mchakato wa mazungumzo kwa niaba ya Serikali ya Burundi. Pia, alisema Uganda haiwezi kuipuuza CNDI badala yake inatakiwa kushirikiana kwa karibu na kamati hiyo.

Chama tawala cha Burundi kilisisitiza kupinga kushiriki kwenye mazungumzo kwa watu waliohusika na jaribio la mapinduzi la Mei mwaka jana.

Uganda ilipanga mazungumzo hayo yafanyike Januari 6 mjini Arusha, lakini Serikali ya Burundi ilisema tarehe hiyo haiendani na makubaliano.


Source: Mwananchi

Comment & Share this!!
Burundi sasa yajadiliwa kimyakimya. Burundi sasa yajadiliwa kimyakimya. Reviewed by Zero Degree on 1/09/2016 05:19:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.