Loading...

Serikali yapunguza makali ubomoaji.


Dar Es Salaam. Wakati athari za bomoabomoa zikizidi kulalamikiwa, Serikali imetangaza hatua ambazo zitapunguza makali ya utekelezaji wa operesheni baada ya mawaziri watatu kukutana kuzungumzia suala hilo.

Operesheni hiyo ilianza kutekelezwa tena juzi kwa kuvunja nyumba zilizoko mabondeni, kwenye kingo za mito, maeneo ya wazi na fukwe za bahari, sambamba na kuweka alama kwenye nyumba zinazotakiwa zibomolewe.

Hata hivyo, operesheni hiyo imepingwa vikali na wananchi kutokana na kuonekana kutojali maisha ya watu licha ya moja ya malengo yake kuwa ni kuwaepusha na janga la mafuriko yanayoweza kusababishwa na mvua za El Nino zinazotarajiwa kunyesha wakati wowote.

Jana, taarifa iliyotolewa baada ya kikao kilichowahusisha Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Tamisemi, George Simbachawene na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, January Makamba ilisema operesheni hiyo itaendelea lakini kwa nyumba zilizo ndani ya mabonde, kwenye miteremko na kingo tu.

“Serikali haina dhamira ya kuwatesa wananchi wake kwa kuwalazimisha kuhama katika makazi yao bila sababu za msingi. Lakini pia Serikali haiwezi kuruhusu wananchi waendelee kukaa katika maeneo ambayo ikinyesha mvua kubwa maisha yao yapo hatarini,” inasema taarifa hiyo iliyotolewa baada ya kikao cha mawaziri hao.

“Zoezi la kuwaondoa wananchi waishio katika Bonde la Mto Msimbazi (eneo hatarishi) litaendelea kwa utaratibu ambao hautaleta mateso na usumbufu kwa wananchi.

“Katika awamu hii, zoezi litajikita katika Bonde la Mto Msimbazi tu... Wale watakaokuwa na nyaraka halali walizopewa na mamlaka za umma, zilizowamilikisha na kuwaruhusu kujenga katika bonde hilo, hawatahamishwa bila kupewa sehemu nyingine za kujenga. Na watumishi wa umma waliowamilikisha maeneo hayo watachukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria.”

Taarifa hiyo inaeleza kuwa, Serikali itaheshimu amri za Mahakama kuhusu mapingamizi yaliyowekwa na baadhi ya wakazi wa mabondeni, lakini pia itafuatilia kesi hizi ziishe haraka ili taratibu zinazofuatia zifanyike.

Kuhusu watumishi wanaoshiriki kuweka alama za “X” kinyume na misingi ya haki, uwazi na kuweka alama kwenye nyumba zilizo nje ya mita 60, Serikali imesema itawachukulia hatua za kinidhamu na imeanzisha dawati la kusikiliza malalamiko ambalo litakuwa Wizara ya Ardhi na Makazi.

Pia, Serikali imesema nyumba na majengo ya miaka mingi, yaliyokuwepo kabla ya kutungwa kwa Sheria zinazotekelezwa kwa zoezi hili, hazitabomolewa isipokuwa tu pale maisha ya wakazi yapo hatarini na kwamba wanaoishi katika makazi hayo watapewa miongozo ya hatua za kuhifadhi mazingira na kujiokoa na maafa.

“Serikali haina dhamira ya kubomoa hoteli kubwa za siku nyingi zilizopo karibu na fukwe katika maeneo ya Masaki, bali wamiliki wake watapewa masharti na miongozo ya kuhifadhi mazingira,” inasema taarifa hiyo.

“Serikali inafuatilia kwa karibu kwa mamlaka za Serikali za Mitaa juu ya taarifa za wananchi wanaohitaji msaada maalumu wa kibinadamu.”

Wakati huohuo, Serikali imesema itamchukulia hatua ofisa wake aliyeshirikiana na mwanasheria wa Mchungaji Getrude Rwakatale kufungua kesi ya kupinga Serikali kuvunjiwa nyumba yake.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa mchungaji huyo alijenga sehemu isiyo sahihi kisheria, lakini aliweka kifusi kuzuia mtiririko wa mto ili kupata eneo zaidi katika miti ya mikoko.

Kadhalika ilibainika kuwa Mchungaji Rwakatare alipata kibali cha NEMC kwa njia ya udanganyifu ili kujenga katika eneo hilo.

“Hapo awali mwanasheria mdogo wa baraza, bila kuagizwa wala kuwaarifu wakubwa zake, Mei 11, 2015, aliingia makubaliano na mawakili wa Mchungaji Rwakatare kwa niaba ya baraza ya kuondoa kesi hiyo mahakamani na kukubali, kwa niaba ya baraza, kutombughudhi kabisa Mchungaji Rwakatare na kusajiliwa kama hukumu ya mahakama Mei 13, 2015,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Hata hivyo, taarifa hiyo ilieleza kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais ilitoa hukumu dhidi ya mwanasheria huyo kwa kumfukuza kazi tangu Januari 6 na taarifa zake kupelekwa Takukuru kwa hatua zaidi.

Kuhusu uhalali wa ujenzi wa karakana ya Mradi wa Mabasi Yaendayo kwa Kasi (DART) kwenye bonde hilo, kikao kiliridhia kuwa ruhusa itolewe katika miradi na shughuli zenye masilahi ya Taifa.


Source: Mwananchi

Comment & Share this!!
Serikali yapunguza makali ubomoaji. Serikali yapunguza makali ubomoaji. Reviewed by Zero Degree on 1/09/2016 05:23:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.