Wasiopeleka watoto shule kutozwa faini ya Sh5 milioni.
Dar es Salaam. Wazazi watakaozembea kupeleka watoto wao shule kuanzia sasa, watahukumiwa kwenda jela miezi sita au kulipa faini ya Sh5 milioni.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Afya na Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu jana, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.
Ummy alisema agizo hilo linatolewa katika kipindi ambacho Serikali inatekeleza Sera ya Maendeleo ya Mtoto ya mwaka 2008 inayosisitiza utoaji wa haki za msingi za mtoto ikiwamo ya kupata elimu.
“Tunaamini kuwa Taifa lililoelimika ni lazima kuwekeza kwenye elimu, ndiyo maana Serikali yetu imetoa elimu ya bure kwa kila Mtanzania pasipo kuwa na ubaguzi wa aina yoyote,”alisema.
Waziri alisema Serikali itahakikisha agizo linasimamiwa kwa kuwa kifungu cha 2 na cha 8 cha Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 vinaeleza kuwa kumpa mtoto elimu ni wajibu wa mzazi au mlezi.
Aliwaagiza viongozi na watendaji wa mikoa na halmashauri kuwasimamia maofisa maendeleo ya jamii na watendaji wa kata kuhamasisha jamii ili watoto wajiunge na darasa la kwanza na kidato cha kwanza, mwaka huu.
“Maofisa maendeleo ya jamii wa mikoa, halmashauri na kata nahitaji msimamie utekelezaji wa agizo hili. Hakikisheni ajenda yenu kuu ni kuhamasisha wazazi kuwapeleka watoto wenye sifa,” alisema.
Alisema, kwa mujibu wa taarifa kutoka Tamisemi, watoto wengi wanatarajia kuandikishwa kuanza masomo ya elimu ya msingi na sekondari, mwaka huu.
Waziri huyo aliwataka wazazi walioathirika na bomoabomoa kuwaandikisha shule watoto wao katika maeneo waliyohamia au kupeleka majina yao wizarani ili yashughulikiwe.
Source: Mwananchi
Comment & Share this!!
Wasiopeleka watoto shule kutozwa faini ya Sh5 milioni.
Reviewed by Zero Degree
on
1/09/2016 05:35:00 PM
Rating: