CDA YAPIGA MARUFUKU shughuli za kilimo maeneo ya makazi.
Kaimu Mkurugenzi wa CDA Paskas Mulagili
Dodoma. Mamlaka ya Ustawishaji Makao Mkuu Dodoma (CDA), imepiga marufuku kilimo kufanyika kwenye maeneo ya makazi ya watu.
Marufuku hiyo ilitolewa jana na Kaimu Mkurugenzi wa CDA, Paskas Muragili alipotembelea eneo la Ilazo lililopo Kata ya Ipagala Manispaa ya Dodoma kujionea uharibifu mkubwa wa ardhi uliotokana na kilimo cha mpunga kwenye viwanja vya makazi.
Alisema wanaofanya hivyo wanakiuka kanuni na sheria ya matumizi bora ya ardhi.
“Eneo hili bado halina mitaro ya kupitishia maji hivyo mvua zinaponyesha maji hujaa na kusababisha usumbufu kwa baadhi ya watu wanaoishi katika maeneo haya. Pia, cha ajabu, kuna baadhi ya watu wanatumia upungufu huo kujinufaisha wao kwa kugeuza mashamba ya mpunga maeneo ambayo maji mengi hutuama licha ya kuwa ni viwanja vya makazi ya watu,” alisema Muragili.
Alionya kuwa mtu yeyote atakayekiuka agizo hilo, atachukuliwa hatua za kisheria.
Hata hivyo, baadhi ya wakulima wanaoendesha kilimo katika eneo hilo, wameilalamikia CDA kwa kuwagawia viwanja hivyo wakati wanatambua vinajaa maji na siyo salama kwa makazi ya watu.
Mkaziwa eneo hilo, Paul Sweya, alisema ameamua kulima mpunga kwenye kiwanja chake baada ya kushindwa kujenga kipindi hiki cha masika.
“Lawama zote ni kwa CDA waliotugawia viwanja hivi kipindi cha kiangazi wakati wanajua kuwa vinajaa maji kipindi cha masika.Kwa hiyo ili kuvilinda visichukuliwe na watu wengine tumeamua kulima mpunga,” alisema Sweya. Hivi karibuni baadhi ya watu wamevamia viwanja vya makazi ya watu vilivyopo Ilazo na kuanzisha kilimo cha mpunga hali iliyosababisha usumbufu kwa wakazi wa eneo hilo kutokana na kuziba kwa mikondo ya maji.
Source: Mwananchi
CDA YAPIGA MARUFUKU shughuli za kilimo maeneo ya makazi.
Reviewed by Zero Degree
on
1/14/2016 02:46:00 PM
Rating: