Loading...

Maalim Seif amwandikia Papa Francis BARUA, pata undani wa barua hiyo hapa.


Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF, Maalim Seif Sharif Hamad

Dar es Salaam. Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amemwandikia barua kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis akitaka atumie ushawishi wake kumaliza mgogoro wa kisiasa Zanzibar.



Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa chama hicho, Ismail Jusa Ladhu alisema jana kuwa makao makuu ya Papa yaliyoko Vatican, bado hayajatoa majibu kwa CUF kuhusu maombi ya barua hiyo.

Barua hiyo imeandikwa wakati jitihada za kumaliza mgogoro wa kisiasa kwenye visiwa hivyo kwa mazungumzo zikionekana kupoteza mwelekeo baada ya wagombea wawili wa urais, Maalim Seif na Dk Ali Mohamed Shein kutoa kauli zinazotofautiana kuhusu hatma ya uchaguzi.

Wakati Dk Shein, ambaye ni Rais wa Zanzibar anayemaliza muda wake, akisema uchaguzi utarudiwa na wananchi wasubiri kutangaziwa tarehe ya kupiga kura, Maalim Seif anasema kurudia uchaguzi ni kubariki vitendo vya uvunjwaji wa Katiba ya Zanzibar na haikubaliki.

Katika barua hiyo ya kurasa mbili, ambayo iliandikwa Novemba 25, 2015 na Mwananchi kuona nakala yake, Maalim Seif ameeleza kile alichodai, jinsi CUF ilivyoshinda chaguzi zote tangu kurejeshwa kwa siasa za vyama vingi mwaka 1995, lakini CCM ikakataa kuiachia iongoze nchi.

Maalim Seif, ambaye amekuwa akigombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF tangu mwaka 1995, amedai katika barua hiyo kuwa kitendo cha watu kutopewa haki zao kwa njia ya uchaguzi kwa kipindi cha miaka 20, kinaweza kusababisha wapoteze uvumilivu na kusababisha baadhi ya vijana kuchukua hatua ambazo ni zaidi ya zile za kidemokrasia. “Ni kwa sababu hizo tunakuomba Mtukufu kutumia ushawishi wako kwa Serikali ya Tanzania ili isitishe mapema hali hii ya kutokuwa na matumaini na kutokuwa na msaada (kabla ya mambo kuwa mabaya),” inaeleza barua hiyo.“Ni wiki tatu tangu uchaguzi ufanyike, na shughuli za kiuchumi zinaelekea kukwama miongoni mwa watu wenye hofu na wanaoangalia mustakabali wa nchi yao, kitu ambacho kinaweza kuchafua utamaduni wetu wa muda mrefu wa kuwa na amani baina ya watu wenye mwingiliano wa dini na utamaduni tofauti.”

Uchaguzi wa Zanzibar ulivurugika Oktoba 28, 2015 baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Jecha Salum Jecha kutangaza kufuta matokeo ya kura za urais, uwakilishi na udiwani, akidai kulikuwa na ukiukwaji wa sheria na kanuni za uchaguzi.

Jecha, ambaye alikuwa akisubiriwa Hoteli ya Bwawani ambako ZEC ilikuwa ikitangaza matokeo, badala yake kuibukia studio za kituo cha televisheni cha Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) kutangaza uamuzi huo, aliahidi kuwa uchaguzi ungerudiwa ndani ya siku 90. Tangazo hilo lilipingwa vikali na Maalim Seif na CUF, akisema matokeo yanaonyesha alishinda uchaguzi na tangu wakati huo imeweka msimamo kuwa haitakubali urudiwe msisitizo ambao pia umo kwenye barua hiyo ya Maalim Seif kwa Papa.

“Hata watetezi wa chama tawala sasa wanakiri kuwa Chama cha Wananchi kimeshinda kila uchaguzi uliofanyika tangu kurejeshwa kwa siasa za vyama vingi mwaka 1995, lakini hakijaruhusiwa kuongoza,” inadai barua hiyo.

“Katika uchaguzi wa mwaka huu, kila timu ya waangalizi wa uchaguzi ilisema kuwa uchaguzi ulikuwa wa amani, huru na wa haki, lakini wakati ilipoonekana kwamba chama tawala kilikuwa kinaelekea kushindwa na matokeo yalishajulikana sehemu nyingi – mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar aliyeteuliwa na rais kutoka chama tawala, ghafla na kwa kutofuata Katiba alibatilisha uchaguzi. “Badala ya kuchukua hatua za kurekebisha kitendo hicho kisicho cha kisheria, Serikali ya Muungano ambako chama tawala kimeshinda, imekuwa ikiisaidia Serikali ya Zanzibar kwa kutumia polisi na vikosi vya jeshi kufanya vitendo vya kutishia.”

Maalim Seif pia amemtaka Papa kutochukulia mgogoro unaotokea Zanzibar kuwa ni wa kidini, bali unaotokana na watu kunyimwa haki zao za kidemokrasia.

“Zanzibar ni nchi ambayo wananchi wake wengi ni Waislamu, kwa hiyo hakuna mgawanyiko wa kidini kabisa. Lakini watu kushindwa kupata haki zao za kidemokrasia kupitia uchaguzi baada ya miaka 20, kunaweza kuwafanya baadhi ya vijana wasioridhika kuchukua njia zaidi ya ile ya kidemokrasia, hali ambayo dunia imekuwa ikishuhudia ikitokea sana siku hizi.”

Katika barua hiyo, Maalim Seif amemweleza Papa historia ya watu wa jamii, tamaduni na dini tofauti kuvumiliana visiwani Zanzibar tangu enzi za utawala wa Sultan, lakini anasema hali hiyo sasa imeanza kupata nyufa.

“Zanzibar imekuwa na historia ndefu ya biashara na uhusiano baina ya tamaduni baina ya watu na dini tofauti ambao unazingatia si tu uvumilivu, lakini kuheshimu tamaduni na dini tofauti kwa miaka maelfu,” anaeleza Maalim Seif katika barua hiyo.

“Wakati Wamishenari wa Kikristo walipomwomba Sultan wa Zanzibar ruhusa ya kujenga kwenye himaya hii mwaka 1840, Sultan wa Kiislamu alimwelezea kuwa ni “mtu wa Mungu anayetaka kueneza neno la Mungu”. “Wakati Zanzibar ilipopata uhuru wake mwaka 1963, kitu cha thamani ya juu kabisa katika kumbukumbu zake kilikuwa kwenye dhima ya uvumilivu wa kidini, kuonyesha makanisa ya Wakatoliki na Waanglikana, misikiti ya Wasuni na Washia na jamatini za Wahindi, ambao wameishi pamoja umbali mdogo kutoka nyumba moja hadi nyingine bila ya kuwa na hofu na migogoro ya kidini.

“Tunasikitika kuwa utamaduni huo wa muda mrefu umeanza kupata nyufa, lakini sababu zinazotolewa mara kwa mara si dini, bali kuondolewa nguvu za kisiasa na kunyimwa haki zetu ambazo haziwezi kutenganishwa nasi. Hapa tunazungumzia uchaguzi wa hivi karibuni uliofanyika Oktoba 25, 2015.”

Akizungumza na Mwananchi jana, Jussa alikiri kuwa walituma barua hiyo kupitia ofisi ya ubalozi wa Vatican na bado hawajapata majibu.



Source: Mwananchi
Maalim Seif amwandikia Papa Francis BARUA, pata undani wa barua hiyo hapa. Maalim Seif amwandikia Papa Francis BARUA, pata undani wa barua hiyo hapa. Reviewed by Zero Degree on 1/14/2016 02:39:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.