Loading...

Wafanyabiashara Moshi kupambana na majambazi wafanyao MAUAJI na UPORAJI.


Moshi. Wafanyabiashara mkoani Kilimanjaro, wamepanga kuunganisha nguvu kuyasaka makundi ya uhalifu yanayotumia bunduki aina ya Shortgun kufanya mauaji na uporaji dhidi yao.

Wakizungumza jana mjini hapa, wafanyabiashara hao wameahidi kutoa fedha kwa ajili ya kuwazawadia raia wema watakaotoa taarifa sahihi za vikundi hivyo.

Hata hivyo, wafanyabiashara hao walioomba majina yao yahifadhiwe wakihofia usalama wao, walisisitiza kuwa vikundi hivyo ni hatari kwani hujeruhi na kuua na wakati mwingine bila kupora chochote.

Walisema kiwango cha fedha kitakachotolewa kwa ajili ya ‘kuwashika mkono’ watakaofanikisha kupatikana kwa silaha na wahalifu hao, kitapangwa na Polisi. “Tunataka tuunganishe nguvu na Polisi wetu maana peke yao hawawezi kufanikiwa. Tunataka watakaosaidia kupata bunduki na wahusika tuwazawadie,” alisema mmoja wa wafanyabiashara hao.

Mwingine alisema vikundi hivyo vinafahamika kwani ni vya watu wanaoishi mitaani, hivyo jamii bado ina wajibu wa kuvifichua.

“Lazima watu wajue kuwa tusipowafichua leo, hawajui kesho nani atavamiwa na kuporwa au hata kuuawa. Nafikiri ni wakati mwafaka kwa wenyeviti wa Serikali za mitaa kuitisha kura za siri kwenye mitaani yao kuwafichua,” alisema.

Mfanyabiashara mwingine, alipendekeza kuundwe kwa kamati za ulinzi na usalama katika mitaa na vitongoji ili kukusanya taarifa za kiitelijensia za uhalifu. Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Ramadhan Mungi alipoulizwa jana, alisema ofisi yake inakaribisha mawazo ya raia wema kukabili uhalifu. Mpango huo umekuja wakati mkuu wa mkoa huo, Amos Makala, leo anakutana na viongozi wa mitaa, vitongoji na vijiji kujadili na kuweka mikakati ya usalama.



Source: Mwananchi
Wafanyabiashara Moshi kupambana na majambazi wafanyao MAUAJI na UPORAJI. Wafanyabiashara Moshi kupambana na majambazi wafanyao MAUAJI na UPORAJI. Reviewed by Zero Degree on 1/14/2016 02:36:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.