Loading...

Sekta za madini, utalii vyakuza pato la Taifa.



Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Dk Albina Chuwa

Dar es Salaam. Imeelezwa kuwa mauzo ya nje ya nchi kwa bidhaa za dhahabu, almasi na madini mengine na utalii, vimechangia kuongezeka kwa pato la Taifa katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 6.3 kutoka 5.4 ya mwaka juzi.



Mbali na bidhaa hizo, ukuaji wa kasi wa shughuli za kiuchumi, mifugo, sekta ya bima, uendeshaji wa Serikali na ulinzi, uzalishaji wa bidhaa za viwandani na uzalishaji wa mazao ya kilimo ni miongoni mwa maeneo yaliyosaidia pia kukuza pato hilo.

Licha ya ongezeko hilo lenye thamani ya Sh71.7 trilioni, bado halikufikia malengo yaliyotarajiwa kutokana na baadhi ya sekta kutofanya vizuri katika robo ya mwaka huo kwa kipindi cha Julai hadi Septemba, ikilinganishwa na mwaka 2014.

Akitoa takwimu hizo jana, Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Dk Albina Chuwa, alisema bado kuna matumaini ya kuongeza thamani ya pato hilo kwa ng’we iliyobaki hadi Desemba 2015.

“Matokeo ya pato la Taifa kwa mwaka 2015 yanayotolewa na Wizara ya Fedha na Mipango kwa mwaka huo, yanakadiriwa kuwa Sh89.1 kwa mwaka mzima, ikilinganishwa na Sh79.4 za mwaka 2014,” alisema Dk Chuwa.

Alisema kutokana na takwimu za pato la Taifa kwa kipindi cha Januari hadi Septemba 2015, kama hakutakuwa na misukosuko ya kiuchumi duniani, matokeo hayo yanatarajiwa kufikiwa.

Alisema kukua kwake kuna maana kwamba Serikali imeendelea kutoa huduma kwa wananchi kama ilivyopangwa.

Akizungumzia kuhusu changamoto ya ukuaji wake, Mwakilishi wa Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI), Hussein Kamote, alisema baadhi ya sekta kama ya viwanda zimekuwa zikikabiliwa na vikwazo vingi.

Alisema bidhaa feki kutoka nje, bandari bubu zinazopitisha mizigo, kusuasua na bei kubwa ya umeme ni sababu zilichochangia kutofanya vizuri kwa sekta.

“Hii mianya ikizibwa na changamoto nyingine kupatiwa ufumbuzi, mchango wa viwanda kwenye pato la Taifa utaongezeka,” alisema Kamote.

Mtaalamu wa masuala ya uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Haji Semboja, alisema licha ya malengo ya kuwa na pato la asilimia nane hadi 10 la kuondoa umaskini, bado halijafikiwa lakini nafasi hiyo ipo. “Dira ni kufikia pato hilo ifikapo 2020/25. Kwa hali ilivyo sasa, tunaweza kufika huko kama changamoto zilizopo zitafanyiwa kazi,” alisema Dk Semboja.




Source: Mwananchi
Sekta za madini, utalii vyakuza pato la Taifa. Sekta za madini, utalii vyakuza pato la Taifa. Reviewed by Zero Degree on 1/14/2016 02:31:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.