Loading...

TFF yawabeba Ngoma, Juuko.


Rais wa TFF, Jamar Malinzi

Dar es Salaam. Wakati Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) juzi ikitoa uamuzi juu ya masuala mbalimbali ya kinidhamu na uvunjaji wa kanuni, shirikisho hilo limeonekana kukosa meno ya kutoa adhabu kwa wachezaji wa Simba na Yanga waliofanya vitendo vya utovu wa nidhamu mwanzo wa msimu huu.

Katika uamuzi huo, timu ya Stand United ilitozwa faini ya Sh500,000 kwa wachezaji wake kupewa kadi tano za njano kwenye mchezo mmoja.

Simba nayo ilitozwa kiasi hicho cha fedha kwa mashabiki wake kufanya vurugu kwenye mechi dhidi ya Mwadui FC, huku wachezaji Fred Mbuna na Hamad Kibopile nao wakipelekwa mbele ya Kamati ya Nidhamu.

Hata hivyo, licha ya shirikisho hilo kuchukua hatua za haraka kwa matukio hayo yaliyotokea hivi karibuni, bado TFF imeendelea kuwa kimya juu ya kesi zinazowahusu Amis Tambwe, Juuko Murshid na Donald Ngoma, ambao malalamiko dhidi yao yalipelekwa mbele ya shirikisho hilo tangu msimu uliopita na mwanzoni mwa msimu huu.

Tambwe alilalamikiwa kwa kumshika korodani Murshid kwenye mechi kati ya Simba na Yanga, Machi mwaka jana, huku Ngoma akituhumiwa kumpiga kichwa beki Hassan Kessy Septemba 26, mwaka jana.

Kwa upande wa Mursheed, anatuhumiwa kumkanyaga makusudi mchezaji Joseph Mahundi wa Mbeya City kwenye mchezo baina ya timu hizo Oktoba 17, mwaka jana.

Bado TFF imekuwa ikisuasua kukaa kwa ajili ya kuwaadhibu wachezaji hao, jambo ambalo limekuwa likilalamikiwa na klabu mbalimbali nchini.

“Kama waliweza kutoa uamuzi wa suala la Juma Nyosso ndani ya kipindi kisichozidi wiki moja, wanashindwa nini kuwaadhibu wachezaji hao, au kwa sababu wanachezea timu kubwa nchini? ” alisema kiongozi wa Mbeya City.

Hata hivyo, TFF imejibu malalamiko hayo ikidai kuwa kamati inayohusika na kesi hizo bado haijakaa na iwapo itafanya hivyo shirikisho hilo litatoa taarifa rasmi.

“Ipo kamati inayoshughulikia masuala hayo na bado haijasema watakaa lini. Wakipanga siku ya kufanya hivyo tutawajulisha watu hawapaswi kuwa na wasiwasi shirikisho linaendeshwa kwa taratibu zake,” alisema Ofisa Habari wa TFF, Baraka Kizuguto.


Source: Mwananchi
TFF yawabeba Ngoma, Juuko. TFF yawabeba Ngoma, Juuko. Reviewed by Zero Degree on 1/14/2016 02:24:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.